Kalonzo alaumiwa kwa ‘kukosesha’ jamii ya Wakamba maendeleo
ALIYEKUWA Seneta wa Kitui David Musila amemtaka Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka akome kukwamisha Ukambani kwenye upinzani na badala yake aruhusu wakazi waunge mkono utawala wa Rais William Ruto.
Bw Musila amesema jamii ya eneo hilo limebakia nyuma kutokana na siasa za Bw Musyoka ambazo zimewaweka katika upinzani baada ya kila uchaguzi mkuu.
Aliongeza kuwa kukwama kwenye upinzani, kumezuia eneo la Ukambani kunufaika kimaendeleo kutoka kwa tawala ambazo huwa zinaingia mamlakani. Hasa alisema Bw Musyoka amewashika mateka kisiasa wakazi wa kaunti za Machakos, Kitui na Makueni na akamtaka awawaachilie ili washirikiane na serikali kwa ajili ya maendeleo.
Seneta huyo wa zamani alidai kuwa baadhi ya viongozi kutoka ngome ya Kalonzo sasa wanatishiwa kwa kufanya kazi na serikali ilhali nia yao ni kuhakikisha wanapata miradi ya maendeleo kwa waliowachagua.
“Namwomba Kalonzo akome kuwashika mateka wanasiasa wa Ukambani na kuwaambia kuwa ndiye Rais 2027. Uongo kama huu ndio umepoteza jamii yetu na kusababisha wakose kupata maendeleo,” akasema Bw Musyoka.
Alikuwa akiongea katika mazishi ya Mutwa Mulindu, 115 kwenye kijiji cha Migwani, Mwingi Magharibi, Kitui mnamo Jumamosi.
Bw Musila alikuwa mwenyekiti wa Wiper lakini akatofautiana kisiasa na Kalonzo mnamo 2017 na akahama chama hicho. Amesema kuwa kiongozi huyo wa Wiper amekuwa kikwazo kwa Wakamba kufanya kazi na serikali kwa miaka 17 iliyopita.
Alitoa mfano wa barabara ya Kitui-Kibwezi-Kabati-Migwani-Mbondoni ambayo imekwama katika eneo la Kwa-Siku kwa muda wa miaka minne kutokana na msimamo wa kisiasa ambao umechukuliwa na Bw Musyoka na baadhi ya viongozi wa Wiper.
Mbunge huyo wa zamani wa Mwingi Kusini alisema kuwa amelazimika amfikie Rais Ruto mwenyewe ili ahakikishe kuwa barabara hiyo ambayo iliachwa baada ya kilomita 25 pekee kuwekwa lami, inakamilishwa.
Kiongozi huyo alisema hata katika demokrasia, baada ya uchaguzi, viongozi walioshindwa hukabili serikali na kupigania maendeleo ya maeneo yao na Wiper inastahili kufanya hivyo.
“Si kazi ya upinzani kuzuia serikali kufanya maendeleo katika ngome zake jinsi ambavyo Wiper imekuwa ikifanya hapa Ukambani. Hili ni kosa kubwa na limetuponza kwa miaka mingi,” akasema.
Alimtaka Kalonzo amuige kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye hushiriki siasa kali wakati wa kampeni na anapolemewa kwenye kura, huvumilia kejeli kisha huungana na serikali kwa ajili ya maendeleo ya ngome zake za kisiasa.
Alisema Raila amedhihirisha hilo kwa kufanya kazi na waliokuwa Marais Daniel Arap Moi, Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta na sasa Rais Ruto.
“Raila ametumia mbinu hii kuhakikisha hakuna kisingizio kuwa maeneo yake hayawezi kufikiwa na serikali kutokana na siasa kali. Hivyo ndivyo Kalonzo anastahili kufanya ili eneo la Ukambani nalo lipate miradi ya maendeleo,” akasema Bw Musila.
Kiongozi huyo alisema kuwa mnamo 2027, wakazi wa Ukambani wana uhuru wa kuchukua mwelekeo wowote wa kisiasa ambao wanaupenda badala ya kulazimishwa kuunga Wiper na uongozi wake.