Kalonzo ashutumu dhuluma za polisi dhidi ya waandamanaji
KIONGOZI wa Azimio la Umoja Kalonzo Musyoka ameshutumu na kulaani vikali kukamatwa na kuteswa kwa waandamanaji waliopinga Mswada wa Fedha wa 2024.
Bw Musyoka alisema Kifungu nambari 37 cha Katiba kimeruhusu watu kuandamana kupinga maongozi mabaya.
“Kama Azimio tunalaani vikali unyama wa polisi dhidi ya Wakenya. Tunawakumbusha polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Nairobi Adamson Bungei kile anajaribu kufanya kuwazuia Wakenya kuandamana kimepitwa na wakati,” Bw Kalonzo alisema punde tu baada ya kuhudhuria maombi ya kumkumbuka hakimu mkazi Monicah Kivuti aliyepigwa risasi katika Mahakama ya Makadara Juni 13, 2024.
Bw Kalonzo alisema inashangaza viongozi wa Kenya Kwanza wanasubiri Rais William Ruto awaite Ikulu ndipo waondoe kodi ya asili mia 16 ya mkate.
“Haya yatakuwa mabadiliko ya mkate. Kwa nini wanakamati ya fedha ya bunge waliongeza kodi?” aliuliza Bw Musyoka.
Kinara huyo wa Azimio alisema hakuna makosa wananchi walifanya kuandamana kupinga Mswada wa Fedha wa 2024/2025.
Alisema gharama ya maisha imeongezeka chini ya uongozi wa Kenya Kwanza na kwamba “vita hivi vya kidemokrasia lazima viendelee. Hakuna anayeweza kuvuruga vita hivi wananchi wameamua kuviendeleza.”
Bw Musyoka alisema Azimio imehuzunishwa na hatua ya polisi kuwatia nguvuni waandamanaji na kwamba itahakikisha kwamba wote waliokamatwa wameachiliwa.
“Hakuna makosa yaliyofanywa na waandamanaji. Katiba imeruhusu maandamano na polisi hawana sababu ya kuwashika waandamanaji,” Bw Musyoka alisema.
“Ni haki ya Wakenya kuandamana na kupinga sheria ama maongozi yanayokinzana na Katiba. Haifai kamwe kwa polisi kutumika vibaya kuwatesa umma,” alisema Bw Musyoka.
Kuhusu kifo cha Bi Kivuti, Bw Musyoka alisema inasikitisha sana kwamba Bi Kivuti alikumbana na mauti akiwa katika harakati zake za kutumikia Wakenya.
Bw Musyoka aliitaka idara ya mahakama ikumbatie uhuru na utekelezaji haki ndipo wawekezaji wawe na imani na nchi hii.
Kinara huyo wa Azimio alitoa wito kwa mawakili na majaji washirikiane kuhakikisha kwamba uhuru wa idara ya mahakama hauvurugwi na yeyote.
Bw Musyoka aliungana na Majaji wa Mahakama ya Rufaa, Mahakama Kuu, Mahakama za Kadhi na Mahakimu kumuomboleza Bi Kivuti aliyekufa kutokana na majeraha ya risasi nne zilizokwama mwilini mwake.
Bi Kivuti alipigwa risasi na aliyekuwa afisa mkuu wa kituo cha polisi Londiani Kaunti ya Kericho Samson Kipchirchir Kipruto.
Kipruto aliuawa papo hapo katika mahakama ya Makadara baada ya kutekeleza uhalifu huo.
Ujumbe wa Jaji Mkuu Martha Koome ulisomwa na Jaji Eric Ogola.
Jaji Koome alimpa sifa sufufu Bi Kivuti na kuahidi kwamba usalama utaimarisgwa katika mahakama zote nchini.
Jaji Koome alipiga marufuku mahakama zote zinazoendelezwa kwenye hema.
Bi Kivuti alihudumu katika mahakama mbali mbali na kupanda gazi kutokana na bidii yake kazini.
Bi Kivuti atakumbukwa kama hakimu shujaa katika utenda kazi wake.