Kalonzo ataka wanaobwagwa kwa urais wapewe ubunge
Na PIUS MAUNDU
KIONGOZI wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka anataka katiba irekebishwe ili kuwawezesha wagombeaji urais wanaoshindwa uchaguzini, wawe wakiteuliwa kuwa wabunge.
Kulingana naye, hali ikiwa hivyo patakuwapo upande wa upinzani wenye nguvu za kufuatilia hatua za serikali.
“Ili kuwepo na upinzani bungeni, yeyote anayewania urais na mgombea-mwenza wake wanafaa pia wawanie ubunge. Kama tungekuwa na hili kwenye katiba, pengine leo ningekuwa Mbunge wa Mwingi Kaskazini na Raila Odinga angekuwa Mbunge wa Lang’ata au Kibra. Tungekuwa tunaongoza vyama vyetu bungeni kwa njia bora zaidi,” alisema mnamo Ijumaa.
Bw Kalonzo anaamini udhaifu wa upinzani uliosababishwa na jinsi katiba ilivyo kwa sasa, ndio umefanya maafisa wengi wa serikali kujitosa katika uporaji wa mali ya umma.
Alizungumza akihutubia wafuasi wake katika Shule ya Msingi ya Mbuuni, Kaunti ya Machakos wakati wa hafla iliyoandaliwa na Mbunge wa Kathiani, Bw Robert Mbui.
Ingawa viongozi waliokuwepo walionekana kutatizwa na jinsi Bw Musyoka anavyokumbwa na uasi katika ngome yake ya Ukambani, alikwepa suala hilo na badala yake kusisitiza kuhusu hitaji la Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kuangamiza ufisadi.
Alilaumu wabunge waliochaguliwa kupitia vyama tanzu vya Muungano wa NASA, pamoja na katiba inayozuia viongozi wa upinzani kuwa wabunge, kwa jinsi ufisadi uilivyokithiri.
“Huwezi kuongoza kikosi chako ukiwa nje lakini tunajitahidi tuwezavyo,” akasema na kutoa wito kwa Wakenya kuunga mkono wito wa kura ya maamuzi.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2017 ambako Bw Musyoka alikuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga aliye Kiongozi wa chama cha ODM, kuliibuka fununu kwamba Mbunge wa Mwingi Kaskazini, Bw Paul Musyimi Nzengu alitaka kujiuzulu ubunge na kumwachia makamu huyo wa rais wa zamani.
Ilidaiwa Bw Nzengu angeteuliwa kuwakilisha Wiper katika Bunge la Afrika Mashariki, na kufanya kuwepo pendo Mwingi Kasikazini ambako Bw Musyoka alikuwa mbunge kwa miaka mingi. Hata hivyo, Bw Nzengu alipuuza ripoti hizo baadaye.
Upande wa upinzani umelaumiwa kwa kukosa nguvu tangu Bw Odinga alipoingia katika mwafaka wa maelewano na Rais Kenyatta mnamo Machi 2018.
Muungano wa NASA ambao ulitoa ushindani mkali dhidi ya Jubilee katika uchaguzi mkuu uliopita, umekuwa dhaifu hasa baada ya Bw Musyoka kumfuata Bw Odinga kushirikiana na serikali, ilhali ilitarajiwa ndiye angejaza pengo lililoachwa na Bw Odinga kuongoza upinzani.
Zaidi ya hayo, vyama tanzu vya NASA vinakumbwa na migogoro ya ndani kwa ndani, ikiwemo kuhusu upande ambao wanachama wanaunga mkono kati ya wanaotetea handisheki na wale wanaomshabikia Naibu Rais William Ruto, anayedai mwafaka huo ni wa kuvuruga mipango yake ya kurithi urais ifikapo 2022.
Ingawa Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi amejitangaza kuwa kiongozi wa upinzani, wadadisi wengi wanahisi hana uwezo wa kujaza pengo lililoachwa na Bw Odinga.