Habari Mseto

Kalonzo aungana na Mawakili kumwambia Ruto aheshimu mahakama

January 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, Ijumaa aliungana na mawakili jijini Nairobi kwenye maandamano ya kumkashifu Rais William Ruto kwa kuishambulia Idara ya Mahakama.

Maandamano hayo yaliandaliwa na Chama cha Mawakili Kenya (LSK) kote nchini, kikilalamikia “kuingiliwa kwa uhuru wa idara hiyo na Rais.”

Maandamano hayo yalianza katika Mahakama ya Upeo, ambapo baadaye yalielekea katika majengo ya Bunge la Kitaifa. Upeo wake utakuwa katika Afisi ya Rais.

Kabla ya maandamano hayo kuanza, Bw Musyoka alitaja matamshi ya Rais Ruto kama tishio kwa mafanikio ambayo yamepatikana katika idara hiyo muhimu, tangu kupitishwa kwa Katiba ya sasa mnamo 2010.

“Tungetaka kumwambia Jaji Mkuu [Martha Koome] na maafisa wenzake kwamba tuko pamoja naye. Hatuko hapa kutafuta mapendeleo yoyote, bali uzingatiaji na utekelezaji wa yale yanayohitaji kutimizwa,” akasema Bw Musyoka.

Akaongeza: “Ikiwa nchi hii haitatawaliwa kwa msingi wa sheria, basi inamaanisha huenda tukaongozwa vile mtu atakavyo.”

Mnamo Januari 2, Rais Ruto aliapa kukaidi maagizo ya mahakama, akidai imekuwa ikitumiwa na baadhi ya watu kuhujumu mipango ya kimaendeleo ya serikali yake.

“Hatutangoja maamuzi ya watu wachache ili kutekeleza mipango tuliyo nayo. Tulipata kibali kutoka kwa wananchi, wala si kwa watu wachache walioketi mahakamani,” akasema Rais Ruto, alipohutubu katika Kaunti ya Nyandarua.

Soma hapa Rais Ruto alivyoshambulia idara ya mahakama: Sitakubali Mahakama Itoe Maamuzi Ya Kukwamisha Miradi Yangu, Ruto Aapa

Maandamano hayo ya Ijumaa yalipoanza, mawakili walicheza densi kwenye barabara za jiji la Nairobi, huku wakiwa wamebeba mabango ya kumkashifu Rais Ruto kutokana na vitisho hivyo.

Baadhi ya mawakili waliojitokeza kushiriki kwenye maandamano hayo ni Ndegwa Njiru, aliyesema kuwa “mambo ni matatu”.

Mawakili wengine waliungana naye kumwambia Rais Ruto kuwa “mambo ni matatu.”

“Mambo ni matatu; heshimu mahakama, heshimu sheria ama uende nyumbani,” akasema Bw Njiru, huku akishangiliwa na mawakili wengine.

Kiongozi wa LSK, Bw Eric Theuri aliwaambia mawakili kuendeleza maandamano hayo wiki ijayo.

“Tunawaomba wanachama wetu wote kushiriki kwenye maandamano tutakayoandaa wiki ijayo wakiwa wamebeba vitambaa vya rangi ya zambarau. Tutasimama kidete na Idara ya Mahakama,” akasema Bw Theuri.

Hayo yanajiri huku mashirika matatu ya masuala ya sheria kutoka Jumuiya ya Madola yakijiunga na mawakili nchini kumkashifu Rais Ruto kwa kuitishia idara hiyo.

Ijumaa, mashirika hayo—Chama cha Majaji na Mahakimu, Chama cha Elimu ya Sheria na Chama cha Mawakili—vilitangaza kuungana na mawakili wa Kenya kuitetea Idara ya Mahakama dhidi ya vitisho kutoka kwa Rais Ruto.

Jaji Mkuu Martha Koome alivyokemea matamshi ya Rais: Koome amjibu Ruto: Ikiwa una ushahidi wa majaji fisadi upeleke JSC