• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Kamala Harris aalika wanawake zaidi kuwania viti vya kisiasa

Kamala Harris aalika wanawake zaidi kuwania viti vya kisiasa

Na MASHIRIKA

BAADA ya kuandikisha historia kama Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke nchini Amerika, Kamala Harris amefunguka na kusema imekuwa kibarua kigumu kwa wanawake kupenyeza kwenye siasa katika mataifa mbalimbali.

Alitaja ushindi wake na Rais mteule Joe Biden kwenye uchaguzi wa wiki jana kama utakaowafungua wanawake macho duniani na kuwawezesha kushiriki siasa ambayo imetawaliwa na wanaume.

Bi Harris akihutubu wakati wa sherehe za ushindi wao katika eneo la Wilmington, Delaware pia aliwashukuru wanawake weusi waliompigia kura kwa kishindo akisema mara nyingi wao hupuuzwa ilhali wao ndio huvumisha demokrasia nchini Amerika.

“Licha ya kwamba, mimi ndiye mwanamke kwenye afisi hii, natambua kuwa sitakuwa wa mwisho. Kila binti mdogo anayetazama anaona nchi hii kama taifa lisilobagua,” akasema.

“Watoto wetu wanafaa wahakikishe wametimiza ndoto zao bila kujali jinsia yao. Huu ni mwamko mpya na kila mwenye nia ya kuwa kiongozi hafai kutupilia ndoto hiyo kutokana na matukio kwenye mawanda ya kisiasa,” akaongeza.

Kwenye hotuba yake Jumamosi usiku, alitambua mchango wa mpiganiaji haki za kibinadamu John Lewis aliyefariki mapema mwaka huu.

Makamu huyo wa Rais mteule alikuwa mwanamke wa nne kuchaguliwa na chama cha kisiasa kuwania kiti cha Urais katika taifa hilo lenye ushawishi mkubwa duniani.

You can share this post!

Uhuru aongoza vigogo wa kisiasa kumpongeza Biden

Ruto aingiwa na baridi kesi yake ya ICC ikifufuliwa