Habari Mseto

Kamata Linturi ikiwa unataka kujitakasa kuhusu mbolea feki, Khalwale aambia Ruto

April 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na SHABAN MAKOKHA

SENETA wa Kakamega, Boni Khalwale, amemtaka Rais William Ruto kudhihirisha hayumo ndani sakata ya mbolea ghushi inayosambazwa kwa wakulima kupitia mpango wa serikali wa mbolea ya ruzuku kwa kuhakikisha wahusika, akiwemo Waziri wa Kilimo Mithika Linturi, wanakamatwa.

Kashfa ya mbolea feki iliwasababishia wakulima hasara waliponunua pembejeo hiyo kwa maandalizi ya msimu wa upanzi mwaka huu.
Seneta Khalwale anamtaka Rais kutoa agizo la kukamatwa kwa waliohusika katika usambazaji wa mbolea hiyo feki akiwemo Bw Linturi ili kuonyesha anatilia uzito malalamishi ya wakulima.

“Itabidi Rais athibitishe anakabili ufisadi kwa kumpiga kalamu waziri huyo na kukamata wote waliohusika katika biashara hiyo haramu ya mbolea feki,” alisema Dkt Khalwale akishangaa kwa nini hatua hiyo imechukua muda mrefu.

Kisha Seneta aliongeza: “Tunataka kila mkulima aliyelaghaiwa na maafisa wa serikali afidiwe. Inasikitisha kuona maafisa wa serikali walio na jukumu la kuhudumia Wakenya ndio wanawaibia.”

Kamati ya Seneti kuhusu Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilisema wakulima walioathiriwa watafidiwa kwa kupewa mbolea ya kuongeza kwenye mimea ili kujaza nakisi ya virutubisho shambani.

Kamati hiyo iliwaita Waziri Linturi, mwenzake wa Biashara Rebecca Miano na maafisa wengine wa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB), Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS), Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) na Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) kueleza kwa nini mbolea feki ilisambazwa katika mabohari ya serikali.

Ikiongozwa na Mwenyekiti Kamau Murango, kamati hiyo ilisema usambazaji wa pembejeo feki kwa wakulima ni sawa na kuhujumu uchumi ama ugaidi na kwamba wahusika wote wanafaa kutiwa nguvuni na kushtakiwa.

Kwa mujibu wa Dkt Khalwale, Wakenya walipopiga kura Agosti 9, 2022, walikusudia kuchagua viongozi ambao wangewahudumia kwa bidii ili kuimarisha maisha yao.

“Wakenya hawakujua kuwa walikuwa wanapigia kura matapeli na wezi ambao wangewaibia wanawake wazee wanaoshinda shambani kutafuta chakula ili kujikimu kwa kuwauzia mawe badala ya mbolea. Itabidi Rais ajiondolee lawama kwa kuchukua hatua kali ya kisheria dhidi ya wahusika,” alisisitiza.

Kadhalika, Dkt Khalwale anapendekeza hatua sawia kuchukuliwa dhidi ya Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa kwa usambazaji wa mbolea feki katika kaunti hiyo. Alisema Bunge la Kaunti lilitenga jumla ya Sh703 milioni za kununua pembejeo feki.

“Nilifichua kwa kuwaita DCI Kakamega wakapata magunia 700 ya mbolea feki katika bohari la Malava. Visa vingine viliripotiwa Ikolomani, Navakholo na sehemu nyingine za kaunti. Lakini sakata hii inafichwa. Tunafuatilia na hatutanyamaza,” akaongezea.

Lakini Waziri wa Kilimo Kaunti ya Kakamega, Benjamin Andama, alishikilia kuwa hakuna mbolea feki iliyosambazwa katika kaunti hiyo.
“Tulifanya uchunguzi kutumia taasisi za utafiti na tukabaini mbolea iliyosambazwa kwa wakulima ilikuwa halisi,” akasema Bw Andama.