Kamishna akana kuhusika katika kashfa ya GAA
Na RICHARD MUNGUTI
ALIYEKUWA kinara wa Tume ya Kuajiri Watumishi wa Umma (PSC) Dkt Alice Atieno Otwala Jumatano alisema hakuhusika na kashfa ya Mamlaka inayosimamia Matangazo ya Serikali (GAA) iliyopelekea Serikali kupoteza zaidi ya Sh122 milioni.
Dkt Otwala alimweleza hakimu mkuu Francis Andayi kwamba hakuandika barua iliyoipa GAA uwezo wa kuchapisha matangazo ya PSC katika Gazeti la The Sunday Express Newspaper linalomilikiwa na Mbunge wa Lugari Ayub Savula aliyeshtakiwa pamoja na wake zake wawili Hellen Kemboi na Melody Gatwiri.
Dkt Otwala alimweleza Andayi kuwa hakuamuru aliyekuwa naibu wake Bw Victor Achola kumwandikia katibu mkuu wa zamani wa Wizara ya Habari, Utangazaji na Teknolojia (ICT) Sammy Itemere akiitaka GAA ichapishe matangazo ya PSC katika Gazeti hilo la Bw Savula.
Kinara huyo aliyepia Kamishna katika Huduma ya Kitaifa ya Polisi (KNPS) alisema “hata sijui kama Gazeti hili- The Sunday Express Newspaper lipo.”
Dkt Otwala alisema “sikumwamuru Achola kuandika barua akiruhusu gazeti hilo kuchapisha matangazo ya PSC.”
Pia alisema hakumwamuru Bw Achola, aliyekuwa mmoja wa maafisa wa habari katika tume ya PSC amwandikie barua Bw Itemere ya kuruhusu mamlaka ya serikali ya kuchapisha matangazo (GAA) kuchapisha matangazo katika gazeti la The Sunday Express Newspaper.
Katika barua hiyo GAA iliruhusiwa malipo ya Sh2,873,660 pamoja na ada ya ziada ya Sh280,000.
Dkt Otwala alisema maafisa wa polisi wa kuchunguza jinai walimpelekea barua hiyo ya Bw Achola na kumwuliza ikiwa anaifahamu na kuwajibu hajawahi iona.
“Mimi sikumwamuru Bw Achola aandike barua hii. Sijui alipata idhini wapi ya kuiandika. Sikumweleza aiandike,” alisema Dkt Otwala.
Hakimu alifahamishwa kuwa utaratibu wa kuandika barua za PSC haukufuatwa kuandika barua hiyo ya Aprili 22, 2016.
Kesi inaendelea.