Habari Mseto

Kamishna aonya walimu dhidi ya kutoza ada haramu za masomo

January 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na Alex Njeru

KAMISHNA wa Kaunti ya Tharaka-Nithi, Bi Beverly Opwora ameonya wasimamizi wa shule katika eneo hilo dhidi ya kutoza ada za masomo kinyume na sheria.

Akihutubia waandishi wa habari mjini Chuka hapo jana, Bi Opwora pia aliwaonya walimu wakuu dhidi ya kulazimisha wanafunzi kurudia darasa au kuwanyima nafasi ya kujiunga na shule zao.

Bi Opwora alisema tayari ameshaunda kamati inayojumuisha maafisa kutoka Wizara ya Ndani na ile ya Elimu na washikadau wengine wa elimu ambao wataangalia hali hiyo kuhakikisha kuwa kanuni za serikali zinazingatiwa kabisa.

“Tunataka kufikia asilimia 100 ya ya wanafunzi kutoka shule za msingi kwenda shule za sekondari bila kuwaadhibu wazazi kwa kuongeza ada,” alisema Bi Opwora.

Alisema baadhi ya waalimu wakuu wako na tabia ya kulazimisha wanafunzi ambao hawafanyi vizuri kaitoa masomo kurudia darasa hasa wale wanaojiunga na darasa la nane na wale wa kidato cha nne ili kupata matokeo mazuri katika mitihani ya kitaifa.

Alishauri pia usimamizi wa shule kukoma kuwalazimisha wazazi kununua sare na vifaa vingine vya watoto wao shuleni au katika duka wanazo pendelea.

“Wazazi au hata wanafunzi wanapaswa kuripoti masaibu yoyote kwa ofisi ya utawala iliyo karibunao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mwalimu yeyoye ambaye hazingatii utaratibu wa serikali,” alisema.

Walimu wakuu wanasema kuwa fedha za serikali hazitoshi kuendeleza shule kwa sababu ya ongezeko la wanafunzi.

Aidha wanasema kuwa shule nyi ngi za sekondari zina shinda ya kushughulikia msongamano kwa sababu ya vifaa vichache vya usafi, mabweni na madarasa ya kufuatia idadi kubwa ya wanafunzi.