Kamishna Kitiyo awaonya wahalifu wanaotumia barakoa kipindi cha janga la Covid-19
Na CHARLES WASONGA
MAGENGE ya wahalifu katika Kaunti ya Mombasa wanadaiwa kutumia barakoa za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona kufunika nyuso zao wanapotekeleza uhalifu.
Kamishna wa Kaunti hiyo Gilbert Kitiyo alisema Ijumaa baadhi ya wahalifu hao pia wanatumia miwani mieusi na kofia kuzuia wasitambuliwe wanapowashambulia wakazi.
Alionya kuwa mbinu hizo bunifu hazitadumu kwani maafisa wa usalama pia wamebuni mikakati bunifu ya kukabiliana na vitendo vya wahalifu hao.
“Tuna habari wanachama wa magenge ya wahalifu wanatumia barakoa wakijifanya wanadhibiti kuenea kwa corona ilhali lengo lao kuu ni kufunika nyuso zao wasitambuliwe wanapotekeleza vitendo vya uhalifu. Mbinu hii haitadumu. Kile ambacho hawafahamu ni kwamba wanaweza kuficha nyuso zao lakini sio sehemu zingine za miili yao,” Bw Kitiyo akawaambia washiriki katika kongomano la kujadili mbinu za kukabiliana na visa vya uhalifu Mombasa.
Alisema maafisa wa usalama wamekuwa chonjo hasa katika kipindi hiki cha janga la Covid-19 hali ambayo imesaidia kupungua kwa visa vya utovu wa usalama katika kaunti nzima ya Mombasa.
Bw Kitiyo pia alielezea matumaini kuwa visa vya uhalifu vitapungua baadaye hata serikali ikiondoa sheria ya kafyu akisisitiza kuwa maafisa wa usalama wataendelea kuwa makini kukabiliana na visa vyovyote vya uhalifu.