Kamishna wa Kiambu awaonya wakandarasi wazembe
WAKANDARASI wamehimizwa kutekeleza wajibu wao jinsi ipasavyo ili kuonyesha utendaji kazi wao kwa serikali.
Kamishna wa Kaunti ya Kiambu Bw Wilson Wanyange, amesema serikali haitawavumilia wakandarasi ambao hufanya kazi duni huku tayari wakiwa wamepokea fedha za miradi.
“Kwa wakati huu serikali iko macho na haitaketi kitako kuona watu fulani wakipokea fedha za kutekeleza miradi za serikali huku wakifanya kazi zao kiholela bila kuwa na umakinifu,” alisema Bw Wanyange.
Alisema kwa muda mrefu wakandarasi wengi ambao wamepewa majukumu ya kuendesha miradi ya serikali wamekuwa na pupa ya kukamilisha miradi ya serikali kwa haraka bila kuonyesha kazi muhimu waliyotekeleza.
Aliyasema hayo mnamo Alhamisi eneo ya Tigoni Kaunti ya Kiambu wakati alijionea mradi wa maji uliogharimu takribani Sh128 milioni.
Aliwahimiza waliopewa kandarasi hiyo wafanye hima kukamilisha mradi huo haraka iwezekanavyo na iwe ni kazi nzuri inayofanywa.
Hata hivyo, ilidaiwa mradi huo ulizinduliwa mnamo Julai 2016, na kukamilishwa 2017!
Kazi yarejelewa upya
Lakini kwa sababu haukukamilishwa kwa umakini kulikuwa na shida kwa usambazaji wa maji na ikabidi kazi hiyo irejelewe upya.
“Ninatoa agizo leo hapa ya kwamba mradi huu sasa ni sharti ufanyiwe kazi inayostahili. Hatutaki kazi zisizo na uhakika. Nikirejea hapa nataka kuona kazi nzuri ya kuridhisha,” alisema Bw Wanyange.
Meneja katika eneo hilo Bi Esther Maina, alipendekeza nyumba za wafanyakazi zijengwe eneo hilo ili watakaoishi hapo waweze kufanya kazi kwa muda wa saa za kuridhisha.
Ninapendekeza nyumba kadha zijengwe hapa ili kurahisisha utendakazi wa wafanyakazi. Mpango huo utaleta mwamko mpya hata kwa wakazi wa Tigoni na vitongoji vyake,” alisema Bi Maina.
Alisema maji ambayo yanasambazwa yanaambatana na ubora wa halmashauri ya NEMA na KEBs pamoja na shirika la afya ulimwenguni (WHO).
Bw Wanyange pia alizuru mradi wa maji Ruiru ambao utagharimu takribani Sh2 milioni, ambao unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.