• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 5:50 AM
Kampuni ya uchukuzi wa umma Thika Road yalaumiwa kwa uendeshaji mbaya wa matatu

Kampuni ya uchukuzi wa umma Thika Road yalaumiwa kwa uendeshaji mbaya wa matatu

Na SAMMY WAWERU

KAMPUNI moja ya usafiri na uchukuzi katika barabara ya Thika Super Highway inalaumiwa kwa uendeshaji mbaya wa matatu.

Zam Zam Sacco, ambayo mabasi yake yanahudumu kati ya mtaa wa Githurai na CBD, jijini Nairobi inatuhumiwa kuwa na utepetevu katika huduma zake.

Hii ni kutokana na maelezo ya majeruhi walionusurika mnamo Jumanne, ambapo basi la kampuni hiyo lenye nambari za usajili KCG 138V linadaiwa kuendeshwa vibaya eneo la Roasters.

Bw James Mwangi, ambaye ni mmoja wa wasafiri waliokuwa katika basi hilo analalamika kupata majeraha mabaya usoni na katika mgongo, wakati wa tukio.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mkazi huyo wa Githurai na aliyekuwa akielekea jijini Nairobi mwendo wa saa kumi na mbili za asubuhi, Jumanne, amesema matatu hiyo ilikuwa ikiendeshwa vibaya na kwa mwendo wa kasi.

“Dereva hakuwa makini, na baadhi yetu tuliokuwa katika viti vya nyuma tulijeruhiwa wakati akivuka matuta kwa kasi eneo la Roasters. Nilipoteza fahamu, na tuliposhuka jijini Nairobi, basi hilo lilitoroka hata licha ya kuarifu afisa mmoja wa polisi,” akasema Bw Mwangi.

Mmoja wa abiria aliyeketi karibu naye alilalamikia maumivu ya mguu.

“Tulilazimika kukodi teksi itupeleke hospitalini. Mwanamume niliyeandamana naye aliteta kushindwa kutembea,” akaelezea.

Anapokea matibabu Nairobi Hospital, na kwa mujibu wa maelezo ya ukaguzi wa daktari aliyemhudumia, alipata majeraha mabaya machoni. Hata hivyo, hospitali hiyo inasema anaendelea kupata nafuu.

Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Kasarani, Nairobi, nambari ya malalamishi ikiwa OB 100/14/5/2019. Kufikia sasa hakuna hatua yoyote imechukuliwa dhidi ya kampuni hiyo ya usafiri.

Taifa Leo imezungumza na mmoja wa mameneja wa Zam Zam Sacco aliyejitambulisha kama Njoro na alisema walipokea malalamishi ya mwathiriwa na kufahamisha mmiliki wa basi hilo.

Si mara ya kwanza kampuni hiyo kunyooshewa kidole cha lawama kwa uendeshaji mbaya wa matatu na utepetevu. Juni 13, mwaka uliopita, 2018, basi linalomilikiwa na Zam Zam Sacco liliripotiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi wa kike wa taasisi ya mafunzo ya elimu ya juu, NIBS, iliyoko Ruiru, Kiambu.

Inadaiwa makanga wa basi hilo lililokuwa likisafiri kwa mwendo wa kasi alisukuma nje mwanafunzi huyo katika eneo la Safari Park.

Alifariki wakati akipelekwa kupokea matibabu katika Hospitali ya Neema, iliyoko mkabala wa mkahawa wa Safari Park.

Visa vya aina hii vinaendelea kushuhudiwa licha ya serikali kuhimiza wamiliki wa matatu kuhakikisha wamezangatia sheria za trafiki, hasa zilizoasisiwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi John Michuki, maarufu kama ‘Michuki Rules’.

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: James Wanjagi Mutwiri

VIWANDA NAKURU: Kampuni zilivyofungwa kwa kulemewa na madeni

adminleo