Habari Mseto

Kampuni yalia wizi wa samaki ukizidi

Na GEORGE ODIWUOR December 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya wakazi wa Suba, Kaunti ya Homa Bay wamegeukia wizi kupata samaki badala ya kutoa jasho au kutumia pesa kupata kitoweo hicho.

Wakazi wa eneo hilo ni wavuvi na baadhi yao kwa miongo kadhaa wamekuwa wakienda ziwani kuvua samaki.

Baadhi ya wakazi wanaozunguka ufuo wa Rowo hata hivyo wameachana na uvuvi majini na badala yake wamegeukia uhalifu wanapopata hamu ya kula samaki.

Baadhi yao huiba kitoweo hicho kutoka kwa mwekezaji wa kibinafsi katika eneo hilo.

Mojawapo wa maeneo ambayo samaki huibwa ni vidimbwi vya Victory Farms, kampuni inayoongoza katika ufugaji wa samaki inayoendesha shughuli zake kutoka Suba.

Kampuni hiyo inazalisha tilapia kwa kutumia vizimba kutoka Ziwa Victoria na ilipewa idhini na Rais William Ruto kupanua uzalishaji kutoka tani 100,000 za sasa hadi tani 150,000 kila mwaka.

Vizimba vyake vingi vya samaki viko katika ufuo wa Rowo.

Baadhi ya samaki pia hufugwa kwenye vidimbwi.

Ni vidimbwi hivi ambavyo baadhi ya wahalifu wamekuwa wakilenga kuiba samaki.

Katika muda wa miezi kadhaa iliyopita, kampuni hiyo imeripoti kupoteza baadhi ya samaki kutoka vidimbwi vyake.Kulingana na Afisa Mkuu wa Maendeleo wa kampuni hiyo, Bw Caesar Asiyo, Victory Farms imechangia pakubwa kupungua kwa uagizaji wa tilapia kutoka China kwa asilimia 50.

Hata hivyo, alizua wasiwasi kuwa kampuni hiyo inapoteza samaki mikononi mwa wezi.Kampuni hiyo ilisema wizi huo unasababisha kudoroa kwa uchumi.

“Maovu haya ni kikwazo sio tu kwa kampuni bali jamii ya wenyeji na Kenya pia. Samaki ndio husaidia kampuni,” Bw Asiyo alisema.

Wizi wa samaki kwa kawaida hufanyika usiku wakati hakuna shughuli zinazofanyika kwenye vidimbwi. Sasa maafisa wa kampuni hiyo wameanza kushirikiana na wenyeji kujaribu kutambua watu wanaohusika na wizi huo.

Bw Asiyo alisema kampuni hiyo imewasiliana na maafisa wa usalama ili kuwasaidia kuangamiza uovu huo.

Alisema idara ya usalama inapaswa kuingilia kati suala hilo.

“Polisi wanapaswa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahalifu. Hii itakuwa mfano kwa wengine wenye nia sawa,” Bw Asiyo alisema.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Suba ya Kati, Bi Beatrice Odira, alisema anafahamu ripoti kuhusu wizi wa samaki kutoka Victory Farms.

Alisema maafisa wa usalama wanashughulikia suala hilo.

“Yeyote anayefanya hivi anafaa kukoma. Maafisa wetu wa usalama wanafanya kila wawezalo kuwanasa washukiwa,” Bi Odira alisema.