Kampuni za mikopo ya pikipiki zapigwa breki kubaini kinachoua wahudumu wa bodaboda
GAVANA Andrew Mwadime ameagiza kampuni mbili maarufu za mikopo ya boda boda kusitisha biashara zao katika kaunti ya Taita Taveta hadi pale uchunguzi dhidi ya mauaji ya wahudumu wa boda boda utakapokamilika.
Hii ni baada ya visa vya mauaji dhidi ya wahudumu wa bodaboda kuongezeka na kuzua taharuki katika kaunti hiyo.
Bw Mwadime amewataka maafisa wa polisi kuchunguza kampuni hizo mbili maarufu kwa kukopa vijana boda boda.
Akiongea kwenye mazishi ya mhudumu wa boda boda aliyeuawa hivi majuzi, Gavana huyo aliamrisha kampuni hizo mbili kusitisha biashara zao katika kaunti yake hadi pale uchunguzi utakapokamilika na ukweli kubainika.
“Kila mmoja asema bodaboda zinazochukuliwa kwa mikopo ikibakia mwezi mmoja au mbili kukamilisha deni la kampuni wahudumu wa biashara hiyo wanakumbwa na mikasa, hasa mauaji au boda boda kuibwa,” alisema Bw Mwadime.
Gavana huyo alisema ipo haja ya kampuni hizo mbili pia kufanya uchunguzi wao ili kuokoa maisha ya wateja wao wanaochukua bodaboda kwa mikopo.
“Boda boda hizo zina teknolojia za kuzifuatilia, mbona zinaibiwa na wahudumu kuuwawa? Wabunge wetu tunawataka mkauliza haya masuala katika Bunge la Kitaifa. Mbona hivi visa vimekithiri hapa Taita Taveta?” aliuliza Bw Mwadime.
Wakati huo huo, aliagiza idara ya leseni kusitisha utoaji wa leseni za boda boda ili uchunguzi ukamilike.