Kampuni za tumbaku lawamani kwa kuvumisha uvutaji wa sigara
Na CHARLES WASONGA
KAMPUNI za tumbaku zimelaumiwa kwa kuendeleza tabia ya uvutaji sigara miongoni mwa vijana kwa kuhimiza uuzaji bidhaa hiyo moja moja kinyume cha sheria kudhibiti matumizi ya tumbaku.
Shirika la International Institute for Legislative Affairs (IILA) ambalo hufuatilia utekelezaji wa sheria hiyo ya 2007 limesema kuwa mwenendo huo umekithiri zaidi katika miji ya mataifa ya Afrika.
Kulingana na sheria hiyo sigara inapasa kuuzwa kwa paketi au “vijiti” visivyopungua kumi.
Nchini Kenya, shirika hilo lilibaini sigara huuziwa moja moja kwa vijana na watu wa mapato ya chini.
“Tuligundua kwama katika maeneo mengine, kampuni za tumbaku bado zinatangaza bidhaa zao, mwenendo ambao umeharamishwa chini ya sheria hiyo,” afisa mkuu mtendaji wa IILA Emma Wanyonyi alisema Jumatano wakati wa kuzinduliwa kwa ripoti kuhusu ukiukaji sheria ya.
Bi Wanyonyi aliwaonyesha wanahabari picha ambazo zilichukuliwa katika kibanda kimoja mtaani Kiberia, Nairobi ikionyesha bango lenye picha ya paketi ya sigara iliyofunuliwa na bei bei ikiwa ni Sh5 kwa kila kijiti.
“Huu mwenendo wa kuuza sigara kwa moja moja unaendeleza uraibu wa uvutaji sigara miongoni mwa vijana, na hata watoto, kwani huwapa ya kujaribu. Hatimaye vijana hao hukolea katika uraibu huo wenye madhara makubwa kiafya,” akasema kwenye kikao na wanahabari katika jijini Nairobi.
Bi Wanyonyi pia alisema idadi ya wanawake wa umri wa chini wanaovuta sigara pia inaongezeka kupitia hatua ya kampuni za tobacco kutengeneza bidhaa zinazowavutia.
“Sigara zenye kiwango cha chini cha ukali, kwa mfano shisha iliyopigwa marufuku na sigara za “kieletroniki” hushabikiwa zaidi na watumiaji wa kike,’ akasema.
Utafiti huo uliendeshwa katika maeneo ya yaliyotengewa wavutaji sigara katikati mwa jiji la Nairobi, na mitaa, kama vile, Kibera, Kileleshwa, Buruburu, Kileleshwa na Karen.
Katika mitaa yenye wakazi wa mapato ya chini wenye maduka walikuwa wakiuza sigara moja moja, bila kufahamu kuwa mwenendo huo ni marufuku kulingana na sehemu ya 18 ya sheria ya kudhibiti matumizi ya tumbaku 2007.