Kampuni za Uchina zapigania majumba mahakamani
Na BERNARDINE MUTANU
Kampuni mbili kutoka China, China Jiangsu inayomilikiwa na Serikali ya China na Ahcof, zinazozana mahakamani kuhusiana na kucheleweshwa kwa ujenzi majumba ya kifahari, Lavington, Nairobi.
Ahcof Investments (Kenya) sasa inataka wakurugenzi wa China Jiangsu kufungwa jela kwa kukataa kumaliza majumba hayo kwa wakati zilizokubaliana.
China Jiangsu pia ilifaa kuweka katika akaunti ya pamoja Sh97 milioni za mawakili wanaowakilisha kampuni hizo mbili.
Ahcof Investment mwaka wa 2017 ilitoa kandarasi kwa China Jiangsu kujenga Astoria Apartments katika barabara ya Mbaazi Avenue, Lavington. Majumba hayo yalifaa kukamilika Machi 2019.
China Jiangsu pia ilitoa Sh97 milioni kama dhamana kwa Ahcof Investment. Pesa hizo zilitolewa na Benki ya Equity.
Ni dhamana hiyo iliyotwaliwa na Ahcof Investment na kufanya China Jiangsu kwenda mahakamani.
“Mshtakiwa wa kwanza (Ahcof) kwa kutumia uongo, kwa siri na utukutu ilimtaka mshtakiwa wa pili (Equity Bank) kuilipa Sh97, 562,888.50 chini ya dhamana ya ufanyikazi ya Novemba 23, 2017 iliyotolewa na kampuni hiyo kwa niaba ya mshtaki,” ilisema China Jiangsu katika hati za mahakama.
Kampuni hiyo ilikana kutotimiza wajibu wake, kwa kusema kuchelewa katika kukamilisha mradi huo kulitokana na nyenzo za ujenzi kutolewa zikiwa zimechelewa na Ahcof, kuchelewa kwa malipo na kuchelewa kwa wanakandarasi walioteuliwa na Ahcof.
Kampuni hiyo ilisema kuwa Ahcof haikujibu maombi ya kurefusha muda wa ujenzi na kusema kuwa haikufaa kutwaa dhamana hiyo kabla ya kutoa jibu.