Kampuni za Uchina zatangaza nafasi 1,000 za kazi kwa Wakenya
Na BERNARDINE MUTANU
Zaidi ya nafasi 1,000 za kazi zimetangazwa na kampuni kutoka China zinazohudumu nchini.
Nafasi hizo zilitangazwa wakati wa kuzindua warsha kubwa ya kazi kati ya Kenya na China na Chama cha Kibiashara (KCETA) Jumatatu.
Katika warsha hiyo, zaidi ya kampuni 50 kutoka China zilifanya maonyesho kwa lengo la kuvutia vijana wanaotafuta kazi.
Nafasi hizo zitakuwa katika sekta za uhandisi, uanahabari na ushonaji.
Kulingana na mkurugenzi wa mashauri ya kigeni Bara Asia na Australia Christopher Chika aliyehudhuria maonyesho hayo, ushirika wa aina hiyo kati ya Kenya na China ni mzuri.
Sio tu unatoa nafasi za kazi, lakini pia unaondoa vikwazo vya kitamaduni kati ya waajiri na waajiriwa.
Alisema kampuni zaidi ya 400 kutoka China zimekuwa zikitoa nafasi za kazi na mafunzo, “hatua nzuri katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya Kenya.”
China itafanya maonyesha ya uagizaji wa kimataifa mwanzoni mwa Novemba kwa lengo la kuimarisha zaidi ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili, alisema Bw Chika.