Habari Mseto

Kanisa la Arise Glory lapongeza hatua ya serikali kufungua shule

October 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY KIMATU

KANISA limepongeza hatua ya serikali ya kuanza kufungua shule baada ya kutangaza kufunguliwa shule kwa watahiniwa wa Darasa la Nane sawia na Kidato cha Nne Jumatatu ijayo.

Hata hivyo, wazazi wamehimizwa kuwatunza watoto waliobakia nyumbani wakati ambapo ratiba ya masomo imetolewa na serikali jana Jumanne.

Hayo yalinenwa Jumanne na Askofu Moses Asiimwe wa Arise Glory Ministries International.

Mhubiri huyo kutoka nchi jirani ya Uganda alionya kwamba huenda kukawa na idadi kubwa ya mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi baada ya kukaa miezi saba bila kuwa shuleni.

“Kuna hatari ya kuwa na ongezeko la visa vya mimba miongoni mwa watoto ifikapo Disemba kutokana na wanafunzi kukaa nyumbani kufuatia janga la corona,” akasema askofu Asiimwe.

Kando na hayo, aliongeza kwamba hospitali, shule na makanisa ni taasisi muhimu na nguzo kuu kwa binadamu ambazo huenda pamoja.

Aliwaomba wakenya kuzingatia kudumisha amani licha ya kuwa na misimamo tofauti ya kisiasa.

Zaidi ya hayo, aliwaonya kujiepusha na vurugu mikutanoni akitoa mfano wa yaliyojiri Murang’a ambapo watu wawili walikufa.

“Mliona jinsi watu wengi walivyopoteza maisha nchini Rwanda kwa tetesi kuwa walitofautiana kisiasa. Chukueni tahadhari za mapema ili tusiende mkondo huo,” akasema.

Hata hivyo, aliwahimiza wakenya kufuata kanuni za wizara ya afya ili wazuie kusambaa kwa virusi vya corona.

Kuhusu matoleo ya wanasiasa makanisani, alidai hakuna makosa pesa kupeanwa kanisani kwa ajili ya huduma ya Mungu.

“Maandiko yamesema vizuri pesa ziletwa kanisani kma matoleo kwa ajili ya kazi ya Mungu wala haijaandikwa zipelekwe barabarani,” askofu Asiimwe akasema.