Kanisa la PEFA Kiambu launga BBI bora majadiliano ya kina yawepo
Na LAWRENCE ONGARO
KANISA la Pentecostal Evangelical of Africa (PEFA), linaunga mkono mpango wa mardhiano (BBI), lakini linataka yawepo majadiliano ya kina.
Kanisa hilo lilieleza ya kwamba ripoti ya BBI haistahili kugawanya Wakenya bali inafaa kuunganisha kila mwananchi.
Askofu John Okinda aliyeongoza wachungaji wengine kutoka maeneo mengine ya Kiambu kutoa maoni yao, alisema maswala yanayozungumzwa kwa mtandao na wananchi kuhusu BBI ni ya kugawanya wananchi.
“Watu wengi wanaotoa maoni yao kuonyesha hasira na hilo haliwezi leta upatanisho kwa vyovyote vile,” alisema Askofu Okinda.
Aliyasema hayo eneo la Juja mnamo Jumatatu walipokuwa wakihutubia waandishi wa habari.
Wachungaji hao wanapendekeza BBI iangazie pakubwa kuhusu maswala ya wanawake.
“Maswala ya jinsia hasa kuwawezesha wanawake yanastahili kuangaziwa ipasavyo,” alifafanua Askofu huyo.
Walisifu mpango wa kuongeza pesa mashinani kutoka asilimia 15 hadi 35 utaleta maendeleo makubwa kwa mwananchi wa chini.
Alitaja ufisadi kama jambo ambalo “limelemaza nchi yetu pakubwa na kwa hivyo ripoti ya BBI inastahili kuliangazia kikamilifu.”
Pia ripoti hiyo imeangazia mpango wa kupanua kazi katika ngazi ya juu huku alitaja kama la busara.
Walitaja kuongezewa kwa mamlaka ya Ombudsman kutalemaza uwezo wa mahakama na kwa hivyo sehemu hiyo inastahili kurekebishwa.
Tume ya IEBC walisema inastahili ijadiliwe zaidi ili iweze kunufaisha kila Mkenya bila mvutano.
“Tungetaka maswala yote ya BBI yawekwe kwa meza ili kusiwe na mvutano wa vikundi viwili. Tungetaka majadiliano yakubalike na kila Mkenya,” alisema Askofu Okinda.
Walipongeza hatua ya kuwa na kiongozi wa upinzani kwenye ripoti hiyo wakitaja hatua hiyo kuwa sawa kwa sababu itafanya serikali kuwa macho inapoendesha shughuli za nchi.
Wachungaji hao kwa kauli moja walitaka serikali kuja na mikakati ya kukabiliana na maradhi ya Covid-19 kwa sababu yanaenea haraka na hivyo kusababisha woga miongoni mwa wanajamii.
Walitaka serikali kuona ya kwamba bima ya NHIF inatumika na mwananchi wa chini “hasa wakati huu tunapokabiliana na Covid-19.”
“Mwananchi wa kawaida hana njia nyingine ya kunufaika na matibabu bali awe na bima hiyo ya NHIF hasa wakati huu mgumu wa homa ya corona,” alisema Askofu huyo.