• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
Kanisa lataka msajili atimuliwe kwa kukataa kupeana hatimiliki

Kanisa lataka msajili atimuliwe kwa kukataa kupeana hatimiliki

NA RICHARD MUNGUTI

SHIRIKA moja la Kanisa la kimataifa linalofadhili shughuli za maendeleo katika nyanja za elimu shuleni, afya hospitalini na ustawi wa kijamii nchini, limewasilisha kesi katika Mahakama Kuu likiomba Msajili Mkuu wa Hatimiliki za mashamba katika Wizara ya Ardhi atimuliwe kazini.

Holistic Mission for All Nations (HMAN) lenye makao yake makuu nchini Korea Kusini linadai katika kesi iliyowasilishwa mahakamani na wakili Lawrence Nyangito kwamba msajili huyo amekataa kupeana hatimiliki ya shamba lililonunua mwaka 2006 kwa bei ya Dola 180,000 (Sh13,580,000).

Katika ushahidi aliowasilisha mahakamani, wakili Lawrence Nyangito alisema msajili huyo amekaidi agizo la mahakama la kuipa HMAN hatimiliki ya shamba hilo la ekari tano lililoko katika mtaa wa kifahari eneo la Muthaiga, Kaunti ya Nairobi.

Wakili huyo alisema mnamo Oktoba 4, 2023, Mwanasheria Mkuu alieleza Jaji Oscar Angote kwamba “hapingi HMAN ikikabidhiwa hatimiliki ya shamba hilo.”

Shirika hilo lilisema limepata pigo kubwa kwa vile haliwezi kutumia ardhi hiyo iliyokusudiwa kutumika kujenga makao yake makuu kuhudumia eneo la Afrika Mashariki na bara nzima.

“Naomba hii mahakama iingilie kati ndipo HMAN ipewe hatimiliki,” Bw Nyangito akasema katika kesi aliyowasilisha katika Mahakama Kuu.

Wakili huyo aliomba korti itoe kibali cha kumtia nguvuni Msajili huyo kisha afikishwe mahakamani na kusukumwa kifungo kisicho chini ya miezi sita gerezani kwa kukaidi agizo la mahakama.

Mahakama pia imeombwa itangaze kwamba mshtakiwa hawezi kuhudumia umma “kutokana na madharau kwa maagizo ya sheria.”

Jaji Oscar Angote aliombwa na HMAN aamuru mali yote ya Msajili huyo ikamatwe na kuuzwa kwa njia ya mnada kugharimia hasara lilopata shirika hilo tangu 2006 liliponunua shamba hilo.

Mahakama ilielezwa kwamba HMAN haijanufaika na shamba hilo kutokana na tabia ya Msajili huyo ya kukataa kupeana hatimiliki.

Kesi hiyo iliwasilishwa na HMAN kupitia kwa msimamizi wake Eun Yon Lee.

Lee alimshtaki Jung Won, Msajili wa Hatimiliki katika Wizara ya Ardhi na Mwanasheria Mkuu.

Jaji Angote alielezwa kwamba agizo alilotoa Aprili 9, 2024, limekandamizwa na msajili ambaye amekataa kuipa HMAN hatimiliki.

  • Tags

You can share this post!

Fainali ya Uefa sasa ni Real Madrid dhidi ya Borussia...

Msako Karatina wanasa washukiwa sita wa kuhangaisha abiria

T L