• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Karata ya Eric Omondi yachanganya wengi

Karata ya Eric Omondi yachanganya wengi

NA WANDERI KAMAU

KWA karibu miaka 15 ambayo amekuwa kwenye ulingo wa sanaa, mcheshi Eric Omondi amekuwa akisifika miongoni mwa Wakenya kutokana na ucheshi wake.

Alijitosa kwenye ulingo wa ucheshi mnamo 2009, kwenye kipindi cha Churchill Live, kilichoanzishwa na mcheshi Daniel Ndambuki, maarufu kama Churchill.

Nyota yake ilipoanza kung’aa, aliondoka katika kipindi hicho na kuanza safari yake kama mcheshi huru.

Alizuru sehemu nyingi barani Afrika na duniani kote kuendeleza kipaji chake.

Hata hivyo, mwelekeo wa mcheshi huyo ulianza kubadilika mwanzoni mwa 2023, alipoanza kuikashifu serikali ya Kenya Kwanza kutokana na matatizo yanayowazonga Wakenya.

Aliwaongoza mashabiki wake mara kadhaa kufanya maandamano jijini Nairobi kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha.

Matokeo ya harakati hizo yalikuwa ni kukamatwa na kuwekwa kwenye seli na polisi.

Mwanzoni, watu wengi walichukulia harakati hizo kama vitimbi na sarakasi za kawaida za mcheshi huyo.

Hata hivyo, siku zilivyoenda, Wakenya walianza kubadilisha dhana zao, wengi wakimwona kwa picha na taswira nyingine isiyo ya mcheshi, bali mwanaharakati wa kijamii.

“Lengo langu ni kutumia umaarufu wangu kuwasaidia Wakenya, maanake wametelekezwa na serikali. Maelfu wanalala njaa huku wengine wakishindwa hata kulipa karo za shule za wanao. Kile nimeanzisha ni harakati za kuwakomboa wananchi kisiasa na kijamii,” akasema majuzi.

Kufikia sasa, Bw Omondi amewasaidia mamia ya Wakenya kupitia mpango anaoita ‘Sisi kwa Sisi’.

Kupitia mpango huo, amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kuwarai Wakenya kuungana kuchanga fedha kuwasaidia watu tofauti wanaojipata kwa shida katika sehemu tofauti nchini.

Baadhi ya shughuli za kuwaokoa raia ambazo amefanya ni kuwasaidia wagonjwa kupata matibabu, ujenzi wa madaraja, kuwasaidia watu kuanzisha biashara, kati ya masuala mengine mengi.

Ijapokuwa mcheshi huyo anasisitiza kuwa hana malengo yoyote ya kisiasa ielekeapo 2027, wadadisi wanasema kuwa kuna uwezekano Bw Omondi anafanya hayo ili kujijengea jina kisiasa.

Katika siku za hivi karibuni, mcheshi huyo ameonekana kuwa na ukaribu mkubwa na kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, na mfanyabiashara Jimmy Wanjigi, ambaye 2022 alikuwa ametangaza nia ya kuwania urais lakini akazuiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Alizuiwa kwa madai ya kutokuwa na shahada ya digrii, kama inavyohitajika kisheria.

Kulingana na Profesa Macharia Munene, ambaye ni mdadisi wa siasa, harakati wa mcheshi huyo ni mbinu za kujiimarisha kisiasa, ikizingatiwa kuwa yeye mwenyewe amekuwa akionekana akitangamana na wanasiasa wa mrengo wa Azimio.

“Ukweli ni kuwa, hatua ya mcheshi huyo kutangamana na viongozi kama Raila au Wanjigi inaonyesha wazi kwamba anatafuta baraka zao kuwania nafasi fulani ya kisiasa. Hilo ndilo lengo lake kuu,” akasema Prof Munene, kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali.

Duru zimekuwa zikieleza kuwa mcheshi huyo analenga kuwania ubunge katika eneo la Lang’ata, 2027, ingawa hajajitokeza wazi kukana au kuthibitisha hayo.

  • Tags

You can share this post!

Afcon 2023: Makocha wa timu zilizozembea wafukuzwa kazi

Masaibu ya wanafunzi wa chekechea wanaofaa kutunzwa kama...

T L