• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Kasisi anayedaiwa kunajisi msichana tineja arejeshwa rumande

Kasisi anayedaiwa kunajisi msichana tineja arejeshwa rumande

NA LAWRENCE ONGARO

KASISI James Kimani Kairu aliyekamatwa akidaiwa kumnajisi mtoto yatima, amerejeshwa rumande dhamana yake ya Sh30,000 ikiondolewa.

Kulingana na hakimu wa Thika Stella Atambo, Kiongozi wa Mashtaka (DPP) na maafisa wa idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) walikosa kufikisha faili ya mshukiwa mahakamani mnamo Machi 4, 2024.

Mshukiwa huyo alikuwa ameachiliwa kwa dhamana ya Sh30,000 lakini aliporejea mahakamani mnamo Alhamisi, faili yake ilikuwa imepatikana.

Hapo ndipo Bi Atambo alifutilia mbali dhamana hiyo ya Sh30,000 na akaamuru mshukiwa kurejeshwa rumande hadi Machi 27, 2024, wakati korti itaamua tena kama atapewa dhamana au la.

Tangu Januari 2024 wakati kesi hiyo ilipofikishwa mbele ya mahakama, hakuna uchunguzi kamili ambao umefanyika na kwa hivyo kuna maswali mengi yanayostahili kuulizwa.

Inadaiwa Kasisi huyo wa Kanisa Katoliki mjini Eldoret alikuwa amemhifadhi mtoto huyo, ambaye ni tineja, katika nyumba fulani ya rafikiye wa kike jijini Nairobi.

Mtoto huyo alitolewa kutoka kituo cha watoto cha Hope Children’s Home mjini Thika mwaka wa 2015 hata kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano

Inadaiwa mshukiwa alikuwa akimnajisi mtoto huyo kisiri katika nyumba hiyo ya rafikiye wa kike.

Alipofikishwa mahakamani, mshukiwa alionekana mtulivu bila kuonyesha wasiwasi wowote akifuatilia kwa makini kikao cha korti.

“Ninaamuru mshukiwa arejeshe rumande hadi Machi 27 ,2024, wakati mahakama hii itatathmini upya dhamana,” akasema Bi Atambo.

  • Tags

You can share this post!

‘Utamu wa safari ya baharini ni abiria kujazana kwa...

Mbunge wa Kenya Kwanza apinga pendekezo la kupandisha bei...

T L