Kassachom motoni
Na CHARLES WASONGA
ALIYEKUWA Katibu wa Wizara ya Afya Khadijah Kassachom anafaa kuadhibiwa kwa kutumia Sh93 milioni zilizonuiwa kugharamia upanuzi wa Hospitali ya Wilaya ya Othaya, Wabunge wamependekeza.
Katika ripoti iliyowasilishwa bungeni Jumatano, wabunge hao ambao ni wanachama wa Kamati ya Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) wanamtaka Bi Kassachom kuelezea Mhasibu Mkuu wa Serikali Edward Ouko sababu zilizosababisha ubadhirifu huo wa pesa hizo za umma kinyume cha Sheria kuhusu Usimamizi za Pesa za Umma ya 2012.
Afisa huyo anahitajika kutoa maelezo hayo katika muda wa miezi mitatu la sivyo alazimishwe kurejesha pesa hizo ambazo ni Sh93,541,451.45.
“Endapo maelezo mwafaka hayatatolewa kwa Waziri wa Fedha na Mhasibu Mkuu katika muda uliowekwa, Bi Khadijah Kassachom anafaa kulazimishwa kulipa pesa hizo alizotumia bila kuzingatia sehemu ya 202 ya sheria ya usimamizi wa fedha za umma ya (PFM Act) 2012,” ikasema ripoti hiyo iliyowasilishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Opiyo Wandayi.
Ingawa Rais Uhuru Kenyatta alimhamisha Bi Kassachom hadi katika Wizara ya Leba kipengee cha 226 (5) cha Katiba kinasema kuwa bado atawajibishwa kwa kosa hilo ikiwa hatawasilisha maelezo kwa Mhasibu Mkuu wa Serikali, Edward Ouko.
Kiipengee hicho kinasema hivi: “Ikiwa mshikilizi wa afisi ya umma, ikiwemo afisi ya kisiasa, ataidhinisha matumizi ya pesa za umma kinyume cha sheria, mtu huyo atawajibikia hasara itakayotokana na kitendo hicho, akiwa afisini au la.
Isitoshe, sehemu ya 68 (1) ya sheria ya usimamizi wa pesa za umma inasema kuwa “afisa mwajibikaji (accounting officer) wa asasi ya serikali ya kitaifa, Tume ya Huduma za Bunge na Idara ya Mahakama atawajibika kwa bunge katika kuhakikisha kuwa rasilimali zilizo chini yake zimetumika kisheria na uwazi.”
Kulingana na ripoti hiyo, Wizara ya Afya alipeana kandarasi ya ustawishaji wa Hospitali ya Wilaya ya Othaya kwa mwanakandarasi mmoja kwa gharama ya Sh436,300,798.
Lakini baadaye gharama hiyo ilipanda hadi Sh501,745,918. Mradi huo ungekamilishw kwa wiki 85 lakini muda huo uliongezwa hadi wikli 123. Hii ina maana kuwa mradi huo ulikamilika mnamo Oktoba 25, 2012.