Habari Mseto

Katibu Mkuu wa KMPDU ajeruhiwa kwenye maandamano jijini

February 29th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

CHAMA cha Kitaifa cha Madaktari Kenya (KMPDU) kimesema kuwa Katibu Mkuu wake, Dkt Davji Atellah, alijeruhiwa vibaya wakati wa maandamano ya kulalamikia kutotumwa kwa madaktari wanafunzi katika sehemu tofauti nchini.

Kwenye taarifa Alhamisi, chama hicho kiliwalaumu polisi, kikisema kuwa Dkt Atellah alikuwa akiongoza maandamano ya amani alipogongwa na mkebe wa gesi ya kutoa machozi na kujeruhiwa.

“Tunawalaumu vikali polisi kwa kumjeruhi Katibu Mkuu wetu, Dkt Atella, alasiri hii alipokuwa akiwaongoza madaktari wanafunzi kwenye maandamano ya amani. Madaktari wa Kenya wamevumilia sana!” kikasema chama kwenye taarifa.

Dkt Atellah alikimbizwa katika Nairobi Hospital, anakoendelea kutibiwa kutokana na majeraha aliyopata.

Katibu huyo alikuwa ameomba kibali cha kuongoza maandamano hayo jijini Nairobi, kwenye barua aliyokuwa amemwandikia Kamanda Mkuu wa Polisi wa Nairobi, Adamson Bungei.

Kwenye barua hiyo, alisema wangefanya maandamano ya amani Alhamisi, kulalamikia kuchelewa kutumwa kwa madaktari wanafunzi na kutolipwa kwa karo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo ya juu.

Madaktari hao waliandamana kutoka makao makuu ya chama hicho katika eneo la Upper Hill hadi katika afisi za Wizara ya Afya. Walikuwa wamepangiwa kuelekea katika makao makuu ya Wizara ya Fedha, katikati mwa jiji.