Habari Mseto

Kauli ya Ndindi Nyoro kwa Raila Odinga

May 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Kiharu katika Kaunti ya Murang’a, Samson Ndindi Nyoro sasa anamtaka Raila Odinga ajishawishi kutekeleza heshima za kimsingi kwa afisi ya Naibu Rais.

Aidha, mbunge huyu ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 38 amehoji ni kwa nini Raila haendi kazini katika afisi ya miundombinu kuhusu muungano wa Afrika (AU).

Lakini cha maana, Nyoro ambaye huiga mtindo wa kusema waziwazi wa mwanasiasa wa Afrika Kusini Julius Sello Malema, amesema kuwa kero yake kuu ni jinsi Raila na viongozi walio upande wake katika siasa za upinzani huwa wanamlenga Ruto kwa maneno na madai ya kila aina kwa nia ya “kumsambaratisha kisiasa.”

Bw Malema ambaye alizaliwa machi 3, 1981, ni mbunge kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) na hujifahamisha na nembo ya kuwa mwingi wa ukali wa hisia za kisiasa na mwepesi wa kusuta wengine.

“Sio lazima aheshimu anayeshikilia wadhifa huo kwa sasa na ambaye ni William Samoei Ruto… Lakini akiheshimu afisi hiyo ambayo imo ndani ya Katiba, atajipata akijizima kukemea Ruto na kumkosea heshima,” akasema Nyoro.

Akiwa mjini Murang’a, Nyoro aliteta: “Raila tangu ajiingize katika mkataba wa handisheki na Rais Uhuru Kenyatta alianza kuonyesha kama aliye na mamlaka makuu ya kikatiba kumliko Ruto.”

“Ningetaka wandani wa Raila au yeye mwenyewe aelezee Wakenya ni wapi Katiba yetu inatambua uongozi ambao hukabidhiwa yeyote kupitia handisheki. Tungetaka watuambie mtu akisalimiana na Rais huwa anatwikwa mamlaka gani ya uongozi,” akasema.

Alimtaka Raila na wandani wake waelewe kuwa katika uchaguzi mkuu wa 2013 na ule wa 2017 kuna Rais aliyechaguliwa hapa nchini na ambaye kwa masharti ya kikatiba, alichaguliwa sambamba na mgombea mwenza ambaye Katiba humtambua kama Naibu Rais.

“Sisi tukitekeleza demokrasia ya kimsingi kama inavyoelekezwa na katiba na ambapo tulichaguana kikatiba, Raila na wenzake walikuwa wanajishughulisha na kukaidi uchaguzi huo ambao uliishia Rais Uhuru na Dkt Ruto kuapishwa kama viongozi wa serikali kati ya 2017 na 2022,” akasema.

Alisema kuwa kinyume na kutii demokrasia kama wanaJubilee walivyofanya, Raila na wafuasi wake walikaidi, wakakataa kushiriki uchaguzi huo wa marudio.

“Raila anafaa awe akijihisi kama aliyepewa hifadhi kama mkimbizi ndani ya serikali na kwa nyakati zote awe akikumbuka kuwa hana uwajibikaji wowote wa kiuongozi ndani ya serikali,” amesema Nyoro.