Kaunti kupokea fedha baada ya Jumanne
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI za kaunti zitaanza kupokea fedha kutoka Hazina ya Kitaifa baada ya Jumanne wiki ijayo.
Hii ni wakati ambapo Bunge la Kitaifa litajadili na kupitisha Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti (CARA),2020, amesema Spika wa muda Christopher Omulele.
Kwenye taarifa kwa wabunge Alhamisi alasiri, Bw Omulele alisema hilo litawezekana baada ya Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti kukamilisha kuchunguza mswada huo na kuwalisha ripoti yake kabla ya Jumatatu, Oktoba 5, 2020.
“Mswada huu ndio utaweka mfumo wa kisheria ambao Hazina ya Kitaifa utatumia kusambaza fedha kwa kaunti katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021,” akasema Spika huyo wa muda ambaye pia ni Mbunge wa Luanda.
Mswada huo utawezesha ugawaji wa Sh316.5 bilioni ambazo zilitengewa kaunti 47 katika bajeti yam waka huu ambao ulisomwa bungeni na Waziri wa Fedha Ukur Yatani.
Usambazaji wa fedha hizo umecheleweshwa kwa miezi mitatu kutokana na vuta nikuvute iliyokuwa ikiendelea miongoni mwa maseneta kuhusu mfumo ufaao kutumiwa katika ugavi wa fedha hizo.
Hali hiyo ilisababishwa kucheleweshwa kupitishwa kwa mswada huo katika Seneti na Bunge la Kitaifa hali iliyopelekea kaunti kukabiliwa na changomoto kuu ya kifedha.
Bw Omulele aliwakumbusha wabunge kwamba ili kuangusha mswada huo hatua hiyo inapasa kuungwa mkono na thuluthi mbili ya wabunge au angalau wabunge 233.