• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
COVID-19: Kaunti ya Kiambu yapata vitanda 400

COVID-19: Kaunti ya Kiambu yapata vitanda 400

Na LAWRENCE ONGARO

GAVANA wa Kiambu Dkt James Nyoro, alizuru hospitali mbili muhimu akiandamana na viongozi kutoka Nairobi.

Gavana wa Kakamega Bw Wycliffe Oparanya ambaye ni mwenyekiti wa baraza la magavana pamoja na Waziri wa Ugatuzi Bw Eugene Wamalwa walizuru Kiambu huku wakitembelea hospitali ya Tigoni na ile ya Wangige; zote zikiwa katika kiwango cha Level 4.

Dkt Nyoro aliwakaribisha viongozi hao ofisini mwake kabla ya kuzuru hospitali hizo.

Kulingana na Dkt Nyoro, hospitali ya Tigoni tayari imepata vitanda 250 nayo Wangige Level 4 imepata vitanda 150 vya wagonjwa walioambukizwa Covid-19.

Gavana huyo alisema Kaunti ya Kiambu imo mbioni kuona ya kwamba inafuata masharti yaliyowekwa na serikali ya kuhakikisha kila kaunti inajiandaa na vitanda zaidi ya 300 ifikapo Julai 6, 2020.

“Kaunti ya Kiambu inataka kuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba inatekeleza agizo la serikali ili kujiandaa mapema kwa mpango wa kukabiliana na Covid-19,” alisema Dkt Nyoro.

Bw Oparanya na Bw Wamalwa walipongeza Kaunti ya Kiambu kwa kuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba inatekeleza wajibu wa serikali.

“Tumeona juhudi zilizofanywa na Kaunti ya Kiambu kwa kuwa na vitanda 400 ili kuiweka tayari kukabili janga la corona. Tunatarajia kaunti zingine zitaiga kuona ya kwamba zinapata vitanda 300 na zaidi ili kujiweka tayari,” alisema Bw Oparanya.

Naye Bw Wamalwa alisema serikali ingetamani kuona mambo yakirejea kama kawaida lakini itategemea jinsi kila mwananchi atakavyokuwa amejitayarisha kukabiliana na janga la corona.

Wakenya wanangoja kwa hamu kusikia uamuzi wa serikali kupitia hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta iwapo atafungua shughuli zirejee kama kawaida.

Hata hivyo, wataalam katika sekta mbalimbali ndio watakuwa na jawabu maalum la kuamua jinsi mambo yatakavyokuwa baada ya Julai 6, 2020.

Sekta ambazo bado zinaipa serikali kiwewe ni elimu na dini.

Sehemu hizo mbili zinahusu mikusanyiko ya watu na kwa hivyo itabidi mikakati maalum iwekwe ili kusije kukawa na taharuki baadaye ya maambukizi au wimbi la pili la maambukizi.

Hata hivyo, sekta ya elimu imekuwa na kizungumkuti kwa sababu hata mpango wa hapo awali wa kufungua shule mwezi Septemba ni wa wasiwasi Huenda pengine shughuli na harakati za elimu shuleni zikarejelewa Januari 2021.

  • Tags

You can share this post!

COVID-19: Wizara yatangaza visa vipya 389 idadi jumla...

Vardy afikisha mabao 100 katika soka ya EPL

adminleo