• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Kaunti yakimbia ‘kuwaokoa’ wanafunzi baada ya vilio vya wazazi

Kaunti yakimbia ‘kuwaokoa’ wanafunzi baada ya vilio vya wazazi

NA WANDERI KAMAU

SERIKALI ya Kaunti ya Nyandarua Alhamisi iliwatuma mafundi kukarabati shule ya chekechea ya Shakora, iliyo eneo la Ngorika, baada ya wakazi kulalamikia hali yake mbaya.

Vyombo vya habari pia viliangazia hali mbaya ya shule hiyo, hali iliyowalazimu wazazi kutoka eneo hilo kuwahamisha wanao na kuwapeleka katika shule nyingine.

Ni wanafunzi watatu tu waliokuwa wameachwa, kwenye jengo hilo, lililoonekana kuwa mahame.

Kabla ya mafundi hao kufika, wanafunzi walikuwa wakilazimika kuvumilia baridi kali, kwani milango, madirisha na hata sakafu hazikuwa zimekamilika kujengwa.

“Nililazimika kumwondoa mtoto wangu kwa kuhofia hali yake ya afya. Hili ni eneo lenye baridi. Hali ya darasa hilo inahatarisha afya yao zaidi, kwani wanafunzi wengi hutoka nyumbani mapema,” akasema Bi Gloria Gathungu, ambaye ni mkazi wa eneo hilo.

Wazazi wengine waliwalaumu maafisa waliokuwa wakisimamia ujenzi huo kwa “kufanya kazi ovyo”.

“Maafisa hao walifaa kufahamu kuwa shule hii ni muhimu kwa eneo hili, kwani hakuna nyingine iliyo karibu. Pili, hili ni eneo la baridi, kwani liko karibu na Milima ya Aberdares,” akasema mzazi mwingine, aliyetambulika kama Wangui.

Hata hivyo, wazazi hao walionekana kuridhishwa na hatua ya kaunti kuwatuma mafundi kukamilisha ujenzi huo, wakisema hilo litawapunguzia pakubwa mzigo wa kuwapeleka wanao katika chechechea zilizo mbali sana.

“Hatimaye tumepata afueni, japo hilo linafaa kuwa changamoto kwa serikali ya kaunti kuhakikisha kuwa shule zote za chekechea ziko katika hali nzuri, kwani ni jukumu lake kusimamia elimu ya msingi,” akaeleza mzazi mwingine.

Kwenye taarifa, kitengo cha mawasiliano katika kaunti hiyo kilisema mafundi wa serikali hiyo wataanza kuzuru kila wadi kuhakikisha kuwa shule zote za chekechea ziko katika hali nzuri.

  • Tags

You can share this post!

Shirika la Barabara Kuu nchini lazindua mpango mkakati

Man U yanyakua afisa mkuu mtendaji wa Man City ili...

T L