Habari Mseto

Kaunti yataka Serikali Kuu ifungue kituo cha madini

February 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LUCY MKANYIKA

SERIKALI ya Kaunti ya Taita Taveta imeitaka Wizara ya Madini na Mafuta kufungua kituo cha madini ya vito cha Voi ili kiweze kuwanufaisha wachimbaji wa eneo hilo na kaunti nyingine jirani.

Akiongea mjini Voi wakati wa hafla ya maonyesho ya madini ya vito, naibu gavana wa kaunti hiyo Bi Majala Mlaghui alisema kuwa kituo hicho kulichomalizika kujengwa mwaka juzi hakijawanufaisha walengwa ilivyokusudiwa.

Kituo hicho kilichogharimu Sh50 milioni kitawezesha wachimbaji wa vito vya thamani kuboresha mawe hayo kabla ya kuyauza.

Wachimbaji huuza mawe yao kwa wanunuzi haswa kutoka nchi za ng’ambo kwa bei ya kutupa na hivyo kupata hasara kubwa licha ya kuchimba mawe katika mazingira magumu.

Mradi huo ulioanzishwa mwaka wa 2015 na aliyekuwa waziri wa Madini Bw Najib Balala ni baadhi ya miradi ya serikali inayonuia kuboresha sekta hiyo ambayo ina uwezo wa kuimarisha uchumi nchini.

“Licha ya kuwa serikali imeleta vifaa na kuwekeza pakubwa katika mradi huu, ni jambo la kusikitisha kuwa bado wachimbaji hawajaweza kunufaika. Tunahimiza serikali kufungua rasmi jengo hili ili liwe la manufaa kama ilivyokusudiwa,” akasema.

Maonyesho hayo yalizileta pamoja kaunti nne zikiwemo Taita Taveta, Kitui, Machakos na Makueni.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na naibu gavana wa Kitui Bw Wathe Nzau, mawaziri mbalimbali wa idara ya madini na maafisa mbalimbali wa kaunti hizo.

Bi Majala alisema kuwa serikali yake itashirikiana na kaunti hizo za eneo la Ukambani ili kuhakikisha kuwa wenyeji wananufaika na raslimali zilizoko ili kuweza kuimarisha maisha yao.

“Tutafanya kazi pamoja ili kuhakikisha kuwa sekta hii inaimarika kwa manufaa ya watu wetu,” akasema.

Aidha, Bw Nzau alikaribisha kaunti ya Taita Taveta kujiunga na muungano wa kaunti za Ukambani (Sereb).

Muungano huo umezileta pamoja kaunti za Kitui, Machakos na Makueni.

“Tuna mambo mengi sana yanayolingana na tukifanya kazi pamoja tutaweza kuyasukuma ili yaweze kuwa ya manufaa kwa wenyeji,” akasema.

Alisema kuwa maeneo ya Ukambani na Taita Taveta yamejaliwa madini ambayo yanaweza kubadilisha maisha ya wenyeji ikiwa kutakuwa na mikakati mwafaka.

Alikubaliana na mwenyeji wake kuwa raslimali hiyo haijakuwa ya manufaa kwa wenyeji ambao wanaishi katika hali ya uchochole.

Kiongozi huyo alisema kwamba uuzaji wa vito kabla ya kusafishwa umekuwa ukiwasababishia wachimbaji hasara kubwa.

“Ninakubaliana na wenzangu kuwa madini yanaweza kuinua uchumi wa nchi na vilevile kuleta maendeleo kwa wananchi. Haya yataafikiwa ikiwa sisi tulio katika maeneo haya tutaweza kushirikiana ili kuhakikisha kuwa tunawezesha wenyeji kuwekeza katika sekta hii,” akasema.