• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:55 AM
Kaunti yatetea ziara ya Uganda iliyoigharimu Sh15 milioni

Kaunti yatetea ziara ya Uganda iliyoigharimu Sh15 milioni

NA DENNIS LUBANGA

SERIKALI ya Kaunti ya Bungoma imetetea safari ya mafunzo ya madiwani na mawaziri wa kaunti hadi nchi jirani ya Uganda wiki jana iliyoigharimu kaunti hiyo Sh15milioni.

Waziri wa Kilimo, Bw Chirasha Makanda  alisema kwamba walijifunza mengi kuhusiana na ujenzi wa viwanda na kuboresha uhusiano kati ya bunge la kaunti na afisi ya gavana.

Bw Makanda alisema safari hiyo ilifaulishwa na Balozi wa Uganda hapa nchini Phoebe Otaala na ililenga kufuatilia tamasha ya utalii na tamaduni iliyoshuhudia ujumbe wa watu 1,000 kutoka Uganda wakiitembelea kaunti ya Bungoma mwaka jana.

Ujumbe uliozuru Uganda kwa muda wa siku nne uliwajumuisha madiwani 61 na baadhi ya mawaziri wa kaunti.

“Watu wetu husema kuona ni kuamini. Ilikuwa jambo la fahari kuona jinsi viwanda vinavyoanzishwa, kuendeshwa na jinsi vinavyochangia ukuaji wa kiuchumi wa eneo,” akasema Bw Makanda.

Kulingana na Mkurugenzi wa mawasiliano wa kaunti Tim Machi, kaunti hiyo imetenga Sh55milioni kwa ujenzi wa kiwanda mjini Webuye, mradi ambao Gavana Wycliffe Wangamati aliahidi kuutekeleza wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2017.

Bw Machi pia alifichua kwamba Sh120milioni zimetengewa uimarishaji wa miundombinu, maji, kuunganishwa kwa nyaya za umeme na kuweka ua katika ardhi ya ekari 103 kwenye eneo la ujenzi wa kiwanda hicho.

Hata hivyo, baadhi ya wenyeji walikashifu madiwani na uongozi wa kaunti kwa kuyafumbia macho matatizo yanayowazonga na kukimbilia kujifunza kuhusu mradi wasiouhitaji kwa sasa.

“Nimevunjika moyo sana na uongozi wa kaunti. Wanakimbia kujifunza kuhusu miradi ilhali watakaoathirika kwa kuhamishwa hawajalipwa fidia wala kuelezwa kuhusu makao yao mapya,” akasema Nancy Nabwire.

  • Tags

You can share this post!

Moses Kuria aongoza wabunge wa Jubilee kuunga mkono Mawathe

Mkutano wa kusuluhisha utata eneo la Kapedo watibuka

adminleo