KAWIRA: Anawanasua vijana kutoka kwa ulevi
Na SAMMY WAWERU
BI Philomena Kawira, mwanadada mwenye kimo cha karibu futi tano ni mwenye ukwasi wa tabasamu na ucheshi.
Ni mtu anayependa kutoa ushauri.
Hata hivyo, Kawira ambaye ni mzaliwa wa Meru ingawa anasukumia gurudumu la maisha kaunti ya Nakuru, ana historia ya maisha ambayo akikutambia utadhani ni zile hekaya za Abunuwasi.
“Wengi nikiwapa ushauri na kuwahadithia niliyopitia wakilinganishe na maisha ya sasa hawaamini,” asema Bi Philomena.
Kulingana na simulizi yake, alianza kubugia mvinyo akiwa shule ya upili, kupitia bintiamu yake.
“Ningemtembelea nyumba yake haikukosa pombe na ndiye alinikaribisha katika utandawazi wa vileo,” asema.
Kilichoanza kama mzaha kilitunga usaha, akawa mtumwa wa vileo.
Anasema alifunguka sawasawa, pombe ikawa sawa na kifungua kinywa ambapo kufikia 2009 alipofanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, Kawira alikuwa akikesha kwenye mabaa na hata vilabuni.
“Nilipojiunga na taasisi ya juu ya elimu, mambo yalinoga,” aelezea. Licha ya wazazi na wanafamilia kumhimiza awe makini, lengo lao likiwa aasi pombe hakuskia la Mwadhini wala mteka maji Msikitini.
Kawira 28, anasimulia kwamba juhudi za wazazi wake kumtafutia kazi Afrika Kusini 2014 ili aoneokane ikiwa ataacha kunywa, ziligonga mwamba kwani maji yalizidi unga. Afrika Kusini ni maarufu katika utengenezaji wa pombe na kuuzwa kwa bei nafuu.
“Huko hata ndio mambo yalizidi,” asisitiza. Miaka mitatu baadaye, Philomena alirejea nchini bila chochote, kwa kile anataja kama kuelekeza mapato yake yote kwa vileo.
Anasema huo ulikuwa mwanzo wa minyororo iliyomshika kufikia kikomo. Shabaha ya kila mmoja ni kuona ameimarika maishani, lakini kwa Kawira ni kana kwamba alikuwa amefumbika macho.
Mwanadada huyu alipotambua zawadi aliyomtunuku Mwenyezi Mungu, uhai, anasema alikata kauli kumtumikia na kumfanyia kazi yake kwa hali na mali. Kulingana naye hali aliyopitia ilimuandaa kutambua kinachoshinikiza watu kunywa, baadhi wakilemewa na hata kufikwa na madhara.
Pombe ni mojawapo ya visababishi vya Saratani, maradhi ambayo yamekuwa kero hapa nchini. Kuna waraibu wa pombe ambao wamepoteza maisha kwa ajili ya kunywa kupindukia.
Isitoshe, baadhi ya wanandoa na familia zimesambaratishwa na suala hili la vileo, wahusika wakilaumiwa kuasi majukumu yao.
Philomena Kawira, amejituma na sasa ni balozi wa kunasua waliotekwa na unywaji wa pombe. “Hasa ninalenga vijana, ambao wameathirika pakubwa. Ninawahamasisha kupitia maisha yangu ya awali, kuwatahadharisha pombe ni hatari na ni gharama,” afafanua.
Kawira anasema akikokotoa hesabu, tangu aanze kunywa ametumia zaidi ya Sh1 milioni kwenye pombe. “Iwapo ningefanya jambo la busara kama vile kujiendeleza kimaisha kwa kuwekeza ningekuwa mbali. Hata hivyo sijafa moyo, ningali mdogo na nina maono makubwa,” aeleza.
Baada ya kusema kwaheri kwa unywaji wa pombe, msichana huyu sasa ana kampuni yake, inayohusika na masuala ya ubadilishanaji wa fedha.
Kasisi Charles Kinyua anasema wengi wanaojitoza katika unywaji wa pombe, kuna msukumo unaowashinikiza. Anataja mawazo, kama mojawapo. Pia, mtandao wa marafiki ni miongoni mwa viini mmoja kujipata katika dimbwi la unywaji vileo, kulingana na Kasisi huyo wa Kanisa la Katoliki.
“Baadhi hujipata kunywa kwa sababu ya masaibu wanayopitia, wanalemewa na mawazo,” asema, akiongeza kuwa malezi yanachangia. Anafafanua kuwa ikiwa mtoto amelelewa katika mazingira ya waraibu wa pombe na hata kutopata ushauri huenda akaishia kujitosa katika visa vya aina hiyo.
“Ni muhimu watoto walelewe kanisani. Wahubiri, Makasisi, Maaskofu na Maimamu, pamoja na viongozi wengine kanisani na washirika huwa katika mstari wa mbele kushauri watoto,” ahimiza Kasisi Kinyua.
Ni busara kushirikiana na waalimu shuleni katika malezi ya mtoto. Wazazi wanashauriwa kutahadharisha wanao dhidi ya makundi potovu.
Kwa upande wake Kawira, anapania kufungua wakfu utakaofanikisha jitihada zake kunasua vijana walioshikwa mateka na unywaji wa pombe, hususan ile haramu.