Habari Mseto

Kazi yenu ni kufinya kompyuta na kuweka pesa kwa mfuko, Ruto aambia vijana wanaotafuta kazi

February 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA LABAAN SHABAAN

RAIS William Ruto ameambia vijana kuchangamkia mpango wake wa kukita vitovu vya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA) ili kujikomboa kutoka kwa lindi la kukosa kazi akiamini watavuna pesa nyingi.

Akizungumza ziarani Kaunti ya Bungoma Alhamisi, Rais mwenye uchu wa kubunia vijana mbinu za kutega uchumi, alikariri mpango wa serikali kujenga vituo vya TEKNOHAMA kuwasaidia kufanya kazi kwenye tarakilishi.

“Tunataka kuwa na vijana kati ya 200 na 300 wanaofanya kazi katika vitovu vya TEKNOHAMA katika kila wadi. Vijana wana kazi mbili: kujitokeza katika vituo hivyo kwa mafunzo na kubonyeza kompyuta na kuweka pesa ya dola za Kimarekani kwa mfuko,” alisema.

Kisha akauliza, “Kwani hii ni ngumu? Kama huwezi kufanya hivyo, mnataka mimi niwasaidie vipi?”

Rais aliahidi wakazi wa Naitiri, eneobunge la Tongaren kuwa atawaundia vituo hivi 6 miezi minne ijayo.

Haya yanajiri majuma mawili tangu Waziri wa TEKNOHAMA na Uchumi Dijitali Eliud Owalo kuzindua vituo dijitali vya Jitume na mtandao wa intaneti (WiFi) katika Chuo cha Kiufundi na mafunzo anuwai cha Bungoma North, Tongaren.

Huu ni mpango mmojawapo wa serikali ya Kenya Kwanza kuinua vijana kiuchumi kupitia njia za kiteknolojia.

Mradi huu wa kutimizwa ndani ya mwongo mmoja (2022 – 2032), umeanza kutekelezwa 2024.

Serikali inalenga kujenga vituo 1,450 kote nchini kupitisha stadi za kidijitali kwa vijana, utayarishaji filamu na kuwezesha umma kupata huduma za serikali kutoka pembe zote za taifa.