KBC yaonywa vikali na chama cha wanahabari
Na MAGDALENE WANJA
CHAMA cha Wanahabari nchini (KUJ) kimetoa makataa ya siku 14 kwa usimamizi wa Idhaa ya Taifa (KBC) kurejesha mpango wa bima ya afya kwa wafanyakazi wake.
Kulingana na maafisa wa KUJ, wafanyakazi wa KBC hawajanufaika na bima ya afya katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Usimamizi wa KBC pia umeshutumiwa kwa kukosa kutuma riba ya kila mwezi kwa taasisi za fedha kulipia mikopo ya wafanyakazi, hatua ambayo imesababisha benki kuwatoza faini.
KUJ sasa imemtaka DPP kuchunguza madai ya ufisadi katika shirika hilo.
“Benki na Sacco sasa zinahangaisha wafanyakazi wa KBC licha ya stakabadhi zao za malipo kuonyesha kuwa walikatwa fedha za kulipia mikopo,” akasema Katibu Mkuu wa KUJ Eric Oduor.
Chama hicho pia kiliitaka wizara ya Habari na Mawasiliano kwa ushirikiano na bodi ya usimamizi ya KBC kuharakisha kuajiri Mkurugenzi Mkuu.
Kulingana na KUJ, KBC imekuwa ikisimamiwa na kaimu mkurugenzi mkuu kwa karibu mwezi mmoja sasa.
“Ili malalamishi ya wafanyakazi yaweze kushughulikiwa kwa haraka, usimamizi wa KBC unafaa kuajiri mkurugenzi mkuu,” akasema mwenyekiti wa KUJ Juma Kwayera.
Bw Kwayera alidai kuwa utawala mbaya na ufisadi vimechangia pakubwa katika kulemaza shughuli katika shirika la KBC. Alimtaka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuchunguza madai ya ufisadi ndani ya shirika hilo na kisha kuwashtaki wahusika.