Habari Mseto

KCB yasema ongezeko la faida ni kutokana na usimamizi bora

November 15th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Benki ya Kenya Commercial imetangaza ongezeko la faida la asilimia 20 katika muda wa miezi tisa kufikia Septemba 30, 2018 ikilinganishwa na wakati huo mwaka wa 2017.

Katika taarufa, KCB ilisema ongezeko la faida hiyo ni kutokana na usimamizi mzuri wa gharama na kuimarika kwa mapato yanayotokana na riba.

“Mapato ya operesheni yaliongezeka kwa asilimia 2 na kufika Sh 54.2 bilioni ambapo mapato yasiyotokana na riba yaliongezeka kwa asilimia 33 kiwango cha jumla cha mapato ya KCB wakati huo,” ilisema KCB katika taarifa.

Kulingana na taarifa hiyo mapato nje ya matawi yaliendelea kuongezeka na kwa sasa ni asilimia 87 ya mapato yake ikilinganishwa na asilimia 13 yaliyopatikana katika matawi yake.

Matumizi ya huduma zake kupitia kwa mawakala yaliongezeka kwa asilimia 74 ilhali idadi ya wananchi waliopata huduma za benki kwa njia ya simu iliongezeka kwa asilimia 34, matumizi ya ATM na maeneo ya kutoa yaliongezeka kwa asilimia 36 na 16 kwa mfuatano huo.

“KCB imekuwa ikiwekeza katika teknolojia kwa lengo la kurahisishia wateja kupata huduma,” ilisema benki hiyo katika taarifa.

Gharama ya operesheni ilipungua kwa Sh2.1 bilioni kutokana na kupungua kwa gharama ya wahudumu wake na mikopo mibaya.

Ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano ilionyesha kuwa kiwango cha kuhifadhi pesa humo kimeongezeka kwa asilimia 6.