• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
KCPE: Aliyepata 376 adaiwa kuuawa baada ya kutahiriwa

KCPE: Aliyepata 376 adaiwa kuuawa baada ya kutahiriwa

Na PETER MBURU

MVULANA wa miaka 15 ambaye alifanya mtihani wa KCPE na kufuzu katika kaunti ya Murang’a aliaga dunia katika mazingira ya kutatanisha, baada ya kudaiwa kuchapwa na wanaume waliokuwa wakipigania kuku, alipopashwa tohara.

Juliano Kanyonyo, 15 alipatikana akiwa maiti katika chumba alimokuwa Jumatatu baada ya kutahiriwa, huku uchunguzi wa maiti yake ukionyesha kuwa huenda aligongwa kichwani na kujeruhiwa akilini.

Watu wa familia ya mtoto huyo ambaye alipata alama 376 katika KCPE walisema kuwa mvulana huyo alichapwa na mwanaume aliyekuwa akimlinda baada ya tohara, kwa kuwa mamake alimpa (mwanaume huyo) kuku ambaye hajakomaa kama malipo kwa watu ambao wangefika kusherehekea hatua hiyo.

Mamake mvulana huyo Beth Nyambura alisema kuwa aliona wanaume wanne wakiingia katika chumba cha marehemu kabla yake kulala usiku wa Jumapili.

Aliongeza kuwa, kuku huyo, ambaye mwanawe alinunua kwa pesa zake baada ya kufanya vibarua alikuwa mdogo na kuwa alipanga kununua mwingine siku iliyofuata.

“Niliporejea nyumbani saa mbili asubuhi, nilibaini kuwa mwanangu hakuwa ameamka ndipo nikaamua kwenda katika nyumba yake, japo ni kinyume na itikadi,” akasema mama huyo.

Alisema kuwa alipoingia alimpata mwanawe kitandani akiwa maiti.

Familia hiyo ilisema kuwa Jumamosi wiki iliyopita, mama huyo alilazimika kumuuza jogoo ambaye alikuwa amemtoa kufanikisha tohara ya mwanawe, baada ya jamaa huyo kulalamika kuwa alikuwa mchanga. “alipoenda sokoni, alimuuza Sh800,” akasema dadake marehemu.

Siku ya mkasa huo, mama huyo alirauka alfajiri kwenda kumtafuta kuku aliyekomaa kijijini, lakini aliporejea ndipo akakumbana na mauti ya mwanawe.

Mtoto huyo aidha anasemekana kuwa alivunjwa mkono wakati alipokuwa akichapwa.

“Uchunguzi wa maiti ulibaini kuwa mvulana aliteswa ndipo akafa,” akasema shangaziye marehemu Juliana Ngami, akisema kuwa wanaume hao wanafaa kushtakiwa.

Mkuu wa polisi eneo la Kandara Wilson Kosgey amesema kuwa polisi wanawasaka wanne hao, japo akipinga kuwa kumekuwa na ongezeko la visa vya wavulana wanaotahiriwa kuteswa.

  • Tags

You can share this post!

Kenya na Mozambique kulegeza kanuni za visa

KRA kunadi magari 568 yaliyokwama bandarini

adminleo