KCPE: Tohara inavyowazuia waliong'aa kusherehekea matokeo
Na PETER MBURU
IMEKUWA furaha ya wanafunzi wengi ambao walifanya mtihani wa kitaifa wa KCPE na kufuzu kusherehekea pamoja na wazazi, walimu na wanafunzi wenzao na kuonekana kitaifa.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wanafunzi kutoka kaunti ya West Pokot, mavuno yao mema yamesherehekewa na wazazi na walimu wao bila ya wao kuwepo.
Hii ni kutokana na hali kuwa wanafunzi hao kwa sasa wanapitia zoezi muhimu maishani mwao, tohara ya kitamaduni, ambayo hawawezi kuonekana kwa muda huu.
Wavulana takriban saba kutoka shule ya msingi ya Kapenguria Town View Academy, akiwemo aliyeongoza kaunti hiyo kwa kupata alama 430 wako eneo fiche kwa tohara hiyo na hivyo matokeo yao yamesherehekewa na familia na walimu tu.
“Tumeweza kupata alama ya wastani 371.26 na mtoto wetu wa kwanza Lokur Ian alipata maki 430, angekuwa pamoja nasi siku ya leo lakini pamoja na wengine wameenda jandoni,” Bi Rebecca Lotuliatum mkuu wa shule hiyo akasema.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wengi kaunti hiyo watajua kuhusu matokeo yao wakiwa jandoni tu, ila ikiwa wameyafurahia ama vingine, hilo umma hautafahamu.
“Mwaka huu tumekuwa na wanafunzi saba ambao wamepata zaidi ya alama 400. Kati ya wanafunzi 43 waliofanya mtihani, hakuna aliyepata chini ya alama 300,” Bi Lotuliatum akasema.
Hata hivyo, baadhi ya wavulana ambao hawakupashwa tohara wamesherehekea matokeo bora pamoja na wazazi wao na kueleza kuhusu ndoto zao.
“Nimefurahia matokeo yangu ya alama 426 na ninatumai kuwa daktari siku za usoni,” akasema Walter Minyonga, mtahiniwa wa mwaka huu.
Shule hiyo ndiyo iliongoza kaunti ya West Pokot.