KCPE: Wazazi wamuua binti yao aliyepata alama 277
Na PETER MBURU
POLISI wanazidi kumsaka baba mmoja ambaye alimpiga bintiye wa miaka 14 hadi kufa kaunti ya Bungoma, baada ya mtoto huyo kulala nyumbani kwa mpenzi wake na kurejea siku iliyofuata.
Inadaiwa kuwa Bw Meshack Baraza alimpa kichapo cha paka mwizi mwanaye ambaye alifanya mtihani wa KCPE mwaka huu na kujizolea alama 277, baada ya mtoto huyo kukosa kurejea nyumbani alipotumwa na mamake Jumapili.
Mtoto huyo alikuwa ametumwa kupeleka pesa kwa mtu wa familia katika kituo cha kibiashara cha Ndalu Jumapili, lakini badala ya kurejea nyumbani akalala nyumbani kwa mpenzi wake na kurejea siku iliyofuata (Jumatatu).
Lakini wazazi wake wanasemekana kumchapa kinyama wakati aliporudi, hadi akafa huku wakitazama.
Mamake mtoto huyo, Bi Gertrude Baraza alikamatwa na polisi nab ado anazuiliwa katika kituo cha Kapchonge kuhusiana na mauaji hayo.
“Nilimpigia mamake simu akaniambia amempata name nikamwambia aniletee mtoto huyo, akasema babake anamchapa,” akasema wifi yake Bi Baraza.
“Nilipopiga simu tena tulizungumza na mtoto mwenyewe ambaye alisema ‘Mama na baba wamenipiga sana, mimi nimekufa, hata wamenifunga Kamba miguu na tumbo’,” akasema mwanamke huyo.
Majirani walisema kuwa walipofika walimpata mtoto katika hali mbaya, huku wazazi wake wakiwazuia kumsaidia, wakati alikuwa akigaagaa kwa uchungu mwingi.
“Nilipata wamechapa huyo mtoto anajivuta chini, wakati alitoka nje akalala na kuitisha maji. Hiyo mvua ilimnyeshea nje yote,” akasema jirani mmoja.
Hata hivyo, matokeo ya KCPE yalipotokea siku aliyouawa baadaye, mtoto huyo alikuwa amefuzu kwa alama 277.
Wazazi hao wanaripotiwa kutenda unyama huo, kwa kuwa walidhani mtoto huyo amepata mimba, kisa ambacho kimekashifiwa kote.