Habari Mseto

Kebs yaweka viwango vipya vya ubora unaohitajika wa mifuko ya kupakia bidhaa

September 24th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

SHIRIKA la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (Kebs), limeweka viwango (standards) vipya vitakavyotoa mwelekeo kuhusu mifuko salama na inayokubalika ya kupakia bidhaa (carrier bags).

Hii ni hatua iliyofikiwa baada ya shirika la Nema kupiga marufuku mifuko ya plastiki mnamo Agosti 2017.

Kiwango hicho cha ubora wa mifuko kinatambulika kama KNWA 2884:2019 Standard na tayari kimependekezwa kuchapishwa na Baraza la Kitaifa la Ubora (NSC) kama njia mojawapo ya kutunza mazingira.

Mkurugenzi mkuu wa Kebs Bw Bernard Njiraini alisema kuwa viwango hivyo vipya vitawapa wanaotengeneza mifuko nafasi ya kufanya biashara bila wasiwasi.

“Kutokana na urahisi wake wa kutumika zaidi ya mara moja na pamoja na kwamba ni ya kutegemewa, mifuko hiyo ilikubalika kuwa bora zaidi,” alisema Bw Njiraini.

Hali mbaya

Hapa awali, Nema ilitoa lalama kuwa kulikuwa na ukosefu wa njia bora ya kutupa taka ambayo imefanya uchafuzi wa mazingira kuwa mbaya zaidi.

Kulingana na Nema, tangu kupigwa marufuku kwa mifuko ya plastiki, kuliibuka viwanda vingi ambavyo hutengeneza mifuko ambayo haifai kwa mazingira.

Vilevile kumekuwepo visa ambapo mifuko ya plastiki bado inatoka mataifa jirani na kuingizwa Kenya kinyume cha sheria.