Kenya haina mafundi wa kutosha – Ripoti
Na WANDERI KAMAU
SEKTA ya kiufundi nchini bado inakumbwa na uhaba mkubwa wa mafundi kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi wanaofuzu kutoka taasisi za kiufundi.
Hilo lilidhihirika Alhamisi kwenye Ripoti Maalum Kuhusu Hali ya Masomo katika Vyuo na Taasisi za Kiufundi nchini iliyotolewa na Wizara ya Leba jijini Nairobi.
Kulingana na ripoti hiyo, asilimia kubwa ya wanaohitimu wanatoka vyuo vikuu, ikilinganishwa na taasisi za kiufundi, hali inayohatarisha lengo la serikali kutimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.
Akihutubu katika uzinduzi huo, Waziri wa Leba, Ukur Yattani alisema kwamba imefikia wakati Wakenya wabadilishe dhana mbaya kuhusu taasisi za kiufundi, kwani hilo ndilo limechangia vijana wengi wanaohitimu kutopata ajira.
“Kudunishwa kwa mafunzo ya kiufundi ndiko kumechangia pakubwa wanafunzi wengi wanaohitimu kutoka vyuo vikuu kukosa ajira, licha ya wengi wao kuwa na shahada. Ni lazima vijana wengi wahimizwe kujiunga na taasisi hizo ili kuhakikisha kwamba wanajiajiri wanapomaliza masomo yao,” akasema Bw Yattani.
Waziri alilalamika kwamba upungufu mkubwa wa mafundi umekuwa mbaya kiasi kuwa serikali imelazimika kuwaajiri raia wa kigeni kuendesha baadhi ya masuala ya kimsingi katika miradi kama ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).
“Inasikitisha kwamba karibu asilimia 90 ya watu wanaoshiriki katika miradi kama SGR wanatoka katika nchi za kigeni kama Uchina. Hili halifai kamwe katika nchi iliyo na vijana wengi na taasisi za kiufundi,” akasema.
Hata hivyo, wizara ilisema itawasilisha ripoti hiyo kwa asasi zingine za serikali ili kuhakikisha kuwa pengo hilo limejazwa.