• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 2:00 PM
Kenya ina uwezo wa kuchunguza coronavirus – Serikali

Kenya ina uwezo wa kuchunguza coronavirus – Serikali

Na Charles Wasonga

KENYA sasa ina uwezo wa kuchunguza na kubaini maambukizi wa ugonjwa hatari wa corona, serikali imetangaza.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe Jumatano aliwaambia wabunge kwamba uwezo huo umethibitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kwa sababu ya idadi ya wataalamu ambao tayari wamepewa mafunzo kuendesha shughuli hiyo na vifaa vilivyoko katika hospitali kuu humu nchini.

“Ningependa kuwahakikishia kwamba Kenya sasa imeungana na mataifa ya Senegal na Afrika Kusini kama mataifa yaliyoidhinishwa na WHO kuwa na vifaa na wataalamu wa kuchunguza coronavirus,” akasema alipofika mbele ya wabunge na maseneta ambao ni wanachama wa kamati kuhusu afya katika majengo ya bunge.

Tangu mkurupuko wa ugonjwa huo kutangazwa na WHO kuwa janga hatari la kiafya, serikali imekuwa ikitumia sampuli za watu wanaoonyesha dalili wa ugonjwa huo nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi.

Bw Kagwe aliongeza kuwa serikali imetoa Sh300 milioni kufadhili mipango ya dharura ya kupambana kuzuia uwezekano wa kutokea kwa maambukizi ya coronavirus humu nchini.

“Na tunatarajia fedha zingine kutoka mashirika ya kifedha ya kimataifa kama vile Benki ya Dunia huku akisisitiza kuwa kufikia sasa hakuna kisa hata kimoja cha ugonjwa huo ambacho kimegunduliwa nchini,” akasema.

You can share this post!

Wabunge wapagawa kwa siasa za 2022

Uhuru hatafika Nakuru kwa mkutano wa BBI

adminleo