Kenya kutumia Sh100 milioni kuokoa raia nchini Lebanon
KENYA inasema imetenga Sh100 milioni kuwaokoa raia waliokwama Lebanon huku vita vikichacha katika nchi hiyo ya mashariki ya kati.
Lakini tarehe halisi za kuokoa bado hazijawekwa kwa Wakenya wanaoonyesha nia ya kurejea nyumbani.
Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni na Wakenya walio ng’ambo, alisema Kenya inafuatilia kwa karibu hali tete nchini Lebanon ambapo Wakenya 26,000 wanafanya kazi na kuishi.
Lebanon imetumbukia katika vita kwa muda wa wiki tatu zilizopita baada ya Israel kuvamia maeneo ya kusini kuwasaka wanamgambo wa Hezbollah.
“Serikali ina wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa raia wetu nje ya nchi, hasa wakati huu wa vita.
“Tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa Wakenya wote katika maeneo yaliyoathiriwa wanahamishwa salama ikiwa hali itazidi kuwa mbaya,” Mudavadi aliambia Seneti Jumatano.
Hatua hii inajiri siku chache baada ya Wakenya waliokwama nchini Lebanon kutoa kilio wakihisi kutelekezwa na serikali, huku mataifa mengine yakianza kuwaondoa raia wao. Kuongezeka kwa mapigano kumeongeza wasiwasi.
“Tunahisi tumekwama, hatuwezi kutoroka. Pasipoti zetu, zinazoshikiliwa na waajiri wetu, ndiyo njia yetu pekee ya kuondoka, lakini wanakataa kuziachilia. Tumekata tamaa. Tunaomba msaada. Tunasihi serikali yetu, na yeyote anayeweza kutusikia—tafadhali tusaidie kurejea nyumbani,” alisema Mary Kamau mfanyakazi wa nyumbani nchini Lebanon.