Kenya Power: Vijiji vyote vitakuwa na pikipiki, magari ya stima kufikia 2025
NA LABAAN SHABAAN
KILA Kijiji nchini kitakuwa na angalau chombo cha usafiri kinachotumia umeme kufikia mwaka wa 2015.
Haya ni malengo ya Kampuni ya Umeme ya Kenya Power inalenga kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya umeme kuendesha mitambo ya uchukuzi.
“Kufikia mwisho wa mwaka wa fedha unaokuja, tunatarajia kuwa na pikipiki ya umeme kila kaunti. Kwa hivyo, kufikia Juni 2025, kila kijiji kitaona bidhaa ya umeme katika mazingira yao. Tunatarajia pia kuwa na angalau gari la umeme kwa angalau nusu ya kaunti mwaka ujao,” alisema Meneja Mkurugenzi wa Kenya Power Joseph Siror.
Kampuni hii itatumia Sh258 milioni kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kukita miundomsingi ya kustawisha uchukuzi kutumia magari ya umeme.
Pesa hizi vile vile zitatumiwa kuunda vituo vya kuchaji magari sehemu mbalimbali nchini pamoja na kununua magari na pikipiki za stima ili kuwezesha oparesheni.
Mnamo Jumatatu, Kenya Power ilizindua kituo cha kumemesha magari chenye gharama ya Sh6.5 milioni katika makao makuu yake Parklands, Nairobi.
Kampuni hii pia ina vituo sawia katika makao yake ya Ruaraka na ina mipango ya kukita vituo vingine 9 ifikapo Julai 2024.
Vituo vya kuchaji magari vitaundwa katika maeneo ya Nakuru, Mombasa, Mtito Andei, Kisumu, Eldoret, na Nairobi (Electricity House, Ragati, Donholm, na Roysambu).
“Mustakabali wa usafiri uko katika umeme. Na sisi kama kampuni tumefurahi kuongoza mazungumzo ya uchukuzi kutumia stima. Pamoja na hitaji letu la kuchaji magari ya umeme, tuna nia ya kutumia vituo vya kuchaji kama sehemu za kunakili takwimu zitakazotusaidia kujua hatua za kukuza sekta ya usafiri kutumia umeme,” Meneja Mkurugenzi wa Kenya Power Joseph Siror alisema.
Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama (NTSA) ilisajili vituo 2,694 mwaka jana, takriban mara sita ya vituo 475 viliyojengwa mwaka uliotangulia.
Kufikia Juni mwaka huu, Kenya Power inalenga kujenga vituo katika miji mikuu Nyeri, Thika, Mombasa, Nakuru, Kisumu, Eldoret, na Nairobi.