Habari Mseto

Kenya, Uganda zaungana kuboresha utalii

April 20th, 2024 1 min read

NA NEHEMIAH OKWEMBAH

WASHIKADAU katika sekta ya utalii kutoka Kenya na taifa jirani la Uganda wameimarisha mipango ya kuboresha uhusiano mwema wa nchi hizi mbili ili kuboresha utalii.

Viongozi katika sekta hiyo waliandaa kongamano maalumu katika hoteli ya Ocean Beach mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi katika msururu wa tamasha ambazo zinanuia kuuza sehemu mbalimbali ili kuvutia watalii kutoka nchi hizi mbili.

Kulingana na washikadau hao, tamasha la Uganda Festival ni mojawapo ya mikakati ya kuimarisha utalii kati ya nchi hizi mbili.

Kulingana na mwakilishi wa nchi ya Uganda eneo la Pwani ya Kenya Paul Mukyumbia, Wakenya 500,000 huzuru nchi ya Uganda kila mwaka na takriban raia wa Uganda 200,000 huzuru Kenya kila mwaka na kuwa idadi hiyo itazidi kuongezeka iwapo uhusiano wa washikadau wa sekta ya utalii wataendelea kushirikiana.

Katibu wa Idara ya Biashara na Utalii katika Kaunti ya Kilifi Herbert Mwachiro alisema kuwa idara hiyo imeanzisha mpango kabambe wa kuuza mila na desturi za jamii ya Mijikenda ili kuweza kuvutia utalii wa nchi mbalimbali.