Kenya yaikokosoa Uchina kuondoa marufuku ya biashara ya pembe za ndovu
Na BERNARDINE MUTANU
SERIKALI ya Kenya imekosoa uamuzi wa China wa kubatilisha marufuku ya biashara ya pembe za ndovu na mifupa ya simba marara.
Wizara ya Utalii na Wanyamapori Ijumaa ilisema kuwa hatua hiyo itawachochea walanguzi wa viungo vya wanyamapori kama pembe za vifaru licha ya upungufu mkubwa wa wanyama hao unaoshuhudiwa nchini.
“Kwa kuzingatia uzoefu wa biashara ya pembe za ndovu na vifaru katika muda wa miaka 25 iliyopita, biashara iliyohalalishwa imeibuka kutokuwa hatua nzuri katika kumaliza uwindaji wa ndovu Afrika. Hatua hiyo itawachochea wafanyibiashara wa bidhaa za pembe,” ilisema taarifa kwa wizara hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa China inatumia imani potovu kwamba pembe za ndovu na vifaru zina dawa licha ya kuwa haijathibitishwa kisayansi.
Kulingana na imani ya baadhi ya watu Asia, pembe za wanyama wa pori zinaweza kutibu baadhi ya magonjwa.
Wizara hiyo ilikuwa ikijibu China baada ya taifa hilo kutangaza kuondoa marufuku ya pembe hizo Jumatatu.
Kulingana na takwimu, kuna vifaru 540 pekee waliosalia nchini, kutoka takriban 20,000 katika miaka ya 1970.