• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Kenya yapokea PPE kutoka WHO

Kenya yapokea PPE kutoka WHO

Na SAMMY WAWERU

KENYA imepokea kutoka kwa Shirika la Afya Duniani, WHO, msaada wa vifaa mbalimbali vya kuwakinga na kuwapunguzia wahudumu wa afya uwezekano wa kuambukizwa virusi vya corona.

Vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh32.1 milioni, vinajumuisha pia maski na vifaa vingine vinavyotumika hospitalini na katika maabara kunakofanyiwa tathmini ya sampuli kubainisha ikiwa mtu ama anaugua Covid-19 au la.

Miungano ya kutetea wahudumu wa afya nchini imekuwa ikilalamikia uhaba wa vifaa vya kujizuia kuambukizwa ugonjwa huo, ikidai baadhi ya wahudumu walioambukizwa na kufariki, maambukizi na maafa yamechangiwa na ukosefu wa vifaa vya kutosha.

Akizungumza Jumatano wakati akitoa taarifa ya maambukizi ya corona nchini, Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya, Dkt Mercy Mwangangi alisema Kenya itawajibikia vifaa hivyo.

“Tangu tuthibitishe kisa cha kwanza cha maambukizi ya Covid-19 nchini, WHO imeendelea kushirikiana nasi. Tunaishukuru kwa msaada wa vifaa hivyo vitakavyotusaidia kupambana na maradhi haya na tutaviwajibikia,” Dkt Mwangangi akasema akiwa katika Afya House jijini Nairobi.

Baadhi ya vifaa vya msaada vilivyotolewa na mfanyabiashara maarufu wa China, Jack Ma mwezi Machi 2020, kusaidia Kenya katika vita dhidi ya corona, mwezi Juni viliripotiwa kupotea katika hali isiyoeleweka, hatua iliyotilia shaka utendakazi wa idara ya afya nchini.

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilianzisha uchunguzi wa sakata hiyo, na kufikia sasa hakuna taarifa iliyotolewa kuhusu kutoweka kwa vifaa hivyo vya msaada.

Mwakilishi wa WHO hapa nchini Bw Rudi Eggers alisema Shirika hilo la Afya Duniani limetoa msaada wa vifaa mbalimbali kuzuia wahudumu wa afya kuambukizwa corona, kwa zaidi ya mataifa 47 Barani Afya, kwa ushirikiano na Muungano wa Kimataifa, ndio UN.

Kwa mara nyingine WHO imeonya mataifa yanayodai kuwa yameshinda vita dhidi ya virusi vya corona, ikisema hatua hiyo ni hatari raia wa nchi hizo.

“Uchumi utarejelea hali ya kawaida tukidhibiti maambukizi,” Bw Rudi akasema, akihimiza umma kutilia maanani sheria na mikakati iliyopendekezwa na shirika hilo na Wizara ya Afya nchini kusaidia kuzuia kuenea kwa Covid-19.

You can share this post!

Hali ya usalama yazorota Mombasa

BURUDANI: Mtunzi anayelenga kuwafaa wasanii chipukizi na...