Habari Mseto

Kero Marsabit mtu mmoja na ng'ombe 200 kuuawa

July 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

VIONGOZI wa Kaunti ya Marsabit wameikejeli serikali kuwa haijawapa wakazi wa kaunti hiyo usalama wa kutosha, baada ya kundi la majambazi kutekeleza mavamizi, na kuua mtu na ng’ombe 200.

Wabunge wa kaunti hiyo walisema vamizi hilo lilitekelezwa eneo la Elebor usiku wa Jumanne, ambapo pia watu wawili na ngombe 600 walijeruhiwa katika makabiliano ya risasi.

Vamizi hilo lilitekelezwa siku moja tu baada ya mmoja wa misururu ya mikutano ya amani ambayo imekuwa ikifanywa na viongozi na wakazi, na wabunge wanalaumu kundi la viongozi fulani kuwa ndio wanachochea jamii fulani kuendeleza fujo.

Wabunge hao aidha walilaumu serikali kwa kuwanyanganya maafisa wa polisi wa ziada bunduki, wakisema wakazi wameachwa bila ulinzi, wakati wakora wa kuiba mifugo bado wanamiliki silaha hizo kwa njia haramu.

“Kuna viongozi katika Kaunti ya Marsabit na katika jamii fulani ambao hawataki kutii mito ya mikutano ya amani ambayo tumekuwa tukiandaa. Baadhi ya viongozi wanachochea watu wa jamii fulani kuendeleza fujo,” mbunge wa Saku Dido Rasso akasema.

Mbunge huyo alisema kuwa japo baadhi ya jamii zimekubali kukaa kwa amani, kunao viongozi wanaowachochea kufanya fujo.

Viongozi hao walilaumu polisi wakisema wanawajua viongozi ambao wanaendeleza fujo hizo, lakini hawajachukua hatua.

“Kwa miezi mingi kama viongozi wa eneo hilo tumekuwa tukifanya juhudi kutafuta amani lakini kuna watu wasiotaka amani Kaunti ya Marsabit,” akasema seneta Naomi Waqo, ambaye pia ni wa kaunti hiyo.