Kesi kuhusu mtaala mpya wa elimu yatajwa ya dharura
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA kuu imeratibisha kesi ya kupinga kuzinduliwa kwa mtaala mpya wa elimu nchini wa 2-6-3-3 kuwa ya dharura.
Jaji Enoch Chacha Mwita (pichani) aliamuru kesi hiyo isikizwe Feburuari 18 na kumwamuru mwanaharakati Okiya Omtatah amkabidhi Waziri wa Elimu Amina Mohammed na Mwanasheria Mkuu (AG) nakala za kesi hiyo.
Jaji Mwita amesema masuala muhimu ya kisheria yameibuliwa na mwanaharakati huyo katika kesi hiyo. Mahakama ilielezwa na wanaharakati Omtatah na Wyclife Chiseba kwamba “Serikali kuu imeamua kuzindua mtaala huu mpya bila kuwasiliana na serikali za kaunti.”
Omtatah aliambia mahakama kwamba serikali imesukuma kutekelezwa kwa mtaala kwa pupa pasi kuweka mikakati na maandalizi yanayohitajika ndipo ufaulu.
Bw Omtatah aliomba mahakama isitishe kabisa kuzinduliwa kwa mtalaa huu mpya hadi maoni ya wananchi yashirikishwe.
“Mlalamishi (omtatah) ameibua masuala mazito ya kisheria kwamba wananchi hawakuchangia katika uzinduzi huu wa mtaala mpya wa elimu kama inavyotakiwa katika katiba,” mahakama ilisema.
Jaji Mwita alisema maagizo anayoomba Omatatah hayawezi kuruhusiwa hadi kesi isikizwe kwa ukamilivu. Alimtaka Bw Omtatah awakabidhi washtakiwa (Bi Amina na AG) nakala za kesi yake ndipo wajibu madai dhidi yao.
Katika kesi aliyowasilisha kortini, Bw Omtatah alisema Waziri amekaidi msururu wa vipengee vya katiba nambari 1, 2, 3(1) na 259 (1) vya katiba vinavyoitaka Serikali isake maoni ya wananchi kabla ya kuzindua mwongozo wowote mpya utakaoathiri maisha yao.
Bw Omtatah anasema katiba imewapa wananchi wa Kenya mamlaka yote ya kueleza jinsi kutekelezwa kwa sheria na kuzinduliwa kwa maongozi mapya.
Mwanaharakati huyu amesema kuwa kifungu nambari 259 kimeeleza wazi wazi kwamba katiba yapasa kutumiwa kustawisha jamii na kufanikisha utekelezaji wa masuala yote ya kusheria.
“Waziri Mohammed amekandamiza katiba na hatua yake yapasa kupigwa breki,” anasema Omtatah katika ushahidi aliowasilisha mahakama kuu.