Habari Mseto

Kesi ya kumtimua Sonko yatajwa kuwa ya kidharura

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI                                          

KUNDI la kinamama Jumatatu liliwasilisha kesi katika mahakama kuu likiomba liunganishwe katika kesi ambapo wakili mmoja anaomba korti imtimue mamlakani Gavana wa Nairobi Mike Sonko.

Kundi hilo linalojulikana kwa jina Divine Sisters linasema Bw Sonko hapasi kuachishwa kazi kwa vile anasaidia makundi ya kina mama na vijana.

Alhamisi wiki iliyopita kesi iliyowasilishwa na wakili Boniface Nyamu liliratibishwa kuwa ya dharura na Jaji Wilfrida Okwany.

Jaji Okwany huyo alisema kuna masuala mazito ya kikatiba yanayostahili kuamuliwa haraka.

Katika kesi aliyoshtakiwa na wakili Boniface Nyamu , gavana huyu anadaiwa ameshindwa kumteua  naibu wake kufuatia kujiuzulu kwa Polycap Igathe.

Pia Bw Nyamu amesema kuwa tabia ya Bw Sonko katika siku za hivi karibuni imekuwa ya kuudhi na anapasa kuchukuliwa hatua kali.

Mahakama imeelezwa mapema wiki hii Bw Sonko aliamuru magari ya uchukuzi wa umma yasiingie kati kati mwa jiji kuwashusha na kuwabeba abiria.

Wakili huyo amesema kuwa agizo hilo la Bw Sonko ilisababisha nchi hii kupata hasara kubwa kiuchumi.

“Nchi hii ilipata hasara kubwa kiuchumi kutokana na agizo la Bw Sonko magari ya uchukuzi wa umma yasiingie katikati mwa jiji,” anasema Bw Nyamu.

Wakili huyo anasema kuwa katiba inawataka magavana wote kuwateua manaibu wao kabla ya kuchaguliwa.

Bw Sonko atawasilisha majibu katika muda wa siku 21.