Habari Mseto

Kesi ya pili ya Sonko yaanza kusikizwa faraghani

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

KESI ya pili ya ufisadi dhidi ya Gavana Mike Sonko inayohusu madai ya ulaji rushwa Sh14 milioni, Jumanne ilianza kusikizwa faraghani katika mahakama ya Milimani, Nairobi.

Hakimu Mwandamizi Peter Ooko alianza kupokea ushahidi kwenye kesi hiyo dhidi ya Sonko aliyeshtakiwa pamoja na Fredrick Odhiambo na Antony Otieno Ombok.

Bw Ooko aliamuru kesi hiyo ianze kusikizwa faraghani baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuondoa ombi la kuwasilisha ushahidi mpya dhidi ya watatu hao

Ombi la kuwasilisha ushahidi huo mpya lilipingwa vikali na mawakili Cecil Miller na George Kithi wanaomwakilisha Sonko.

Akipinga ombi la DPP kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Bw James Kihara, Bw Miller alisema ni ukiukaji wa haki za Bw Sonko kupewa ushahidi mpya wakati kesi imeorodheshwa kuanza kusikizwa.

Hakimu alikubaliana na wakili Miller na kusema tayari aliratibisha ombi la DPP kuwa la dharura.

Wakili Paula Atikuda alipinga vikali uwasilishwaji wa ushahidi mpya na kusema DPP amekaidi agizo la mahakama kwamba hakuna ushahidi mpya utakubaliwa kuwasilishwa kesi ikianza kusikizwa.

Mahakama Kuu iliamuru awali kuwa ushahidi wote uwe ukikabidhiwa washtakiwa siku saba kabla ya kesi kuanza kusikizwa.

Bw Ooko aliwaruhusu mawakili wa Sonko wawasilishe ombi katika Mahakama Kuu kupinga kuendelea kusikizwa kwa kesi hiyo.

Wiki mbili zilizopita, Hakimu Mkuu Douglas Ogoti alianza kupokea ushahidi faraghani wa kesi nyingine dhidi ya gavana huyo ya rushwa ya Sh10 milioni.