KFCB kushtaki runinga zinazopeperusha matangazo ya kondomu
Na PETER MBURU
MWENYEKITI wa Bodi ya Kusimamia na Kukadiria Uainishaji wa Filamu nchini (KFCB) Ezekiel Mutua ameelezea kughadhabishwa kwake na tangazo la kibiashara linalopeperushwa katika runinga za humu nchini kuhusu mipira ya kondomu.
Bw Mutua ambaye amejishindia sifa ya kuwa ‘kachero wa maadili’ machoni pa Wakenya alisema tangazo hilo limekuwa likipeperushwa wakati familia zinatazama runinga, hivyo kuishia kupeperusha habari zisizowiana na maadili.
Bw Mutua alisema tangazo hilo, ambalo mipira ya kondomu imepewa jina ‘soksi’ limekuwa likipeperushwa nyakati zinazotazamwa zaidi jambo ambalo wazazi hawajaridhishwa nalo.
“Kufuatia malalamiko kutoka kwa Wakenya wengi kuhusu tangazo la kondomu ‘soksi’ ambalo linapeperushwa na televisheni nyingi nyakati zisizoruhusiwa, bodi ilianzisha uchunguzi kuhusu suala hilo na ikabaini kuwa tangazo hilo halikuwasilishwa ili kukaguliwa kulingana na sheria,” akachapisha Bw Mutua kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumatatu jioni.
Alisisitiza kuwa kupeperushwa kwa tangazo hilo kulikiuka sheria, akisema wanaolipeperusha watakabiliwa vilivyo.
“Bodi imetoa maelekezo kwa mawakili wake kuendelea kushtaki vituo vinavyopeperusha matangazo kwa kukiuka sheria. Kfcb itatoa habari kamili kuhusu suala hili,” akasema Bw Mutua.