• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
KFCB yachukua hatua kuzima magari ya umma yanayoonyesha filamu bila leseni

KFCB yachukua hatua kuzima magari ya umma yanayoonyesha filamu bila leseni

Na DIANA MUTHEU

BODI ya kutathmini Ubora wa Filamu Nchini (KFCB) imeanzisha msako kote nchini dhidi ya magari ya umma yanayoonyesha filamu na muziki wenye maudhui chafu.

Akizungumza na ‘Taifa Leo’ katika ofisi kuu ya Nairobi, Jumatatu, Mkurugenzi wa KFCB Ezekiel Mutua alisema kuwa magari haya yanaonyesha filamu hizi kinyume na sheria hata baada ya onyo kutolewa mnamo Februari, 2018 baada ya mikutano kadhaa baina ya bodi hii na vyama vya matatu na mabasi.

Dkt Mutua alisema kuwa wamepata malalamishi kutoka kwa wasafiri kote nchini kuwa filamu ambazo magari ya umma yanaonyesha zinaweza kuharibu maadili ya watoto.

“Madereva na makondakta hawa wanavunja sheria, lakini pia wanaonyesha watoto wadogo filamu chafu. Wazazi wengi wameelezea jinsi ambavyo wamevumilia sana kusafiri pamoja na watoto wao katika magari hayo,” alisema Dkt Mutua.

KFCB ilitangaza kuwa magari yote ambayo yana televisheni yako katika kitengo cha ‘mashirika’ yanayoonyesha filamu na hivyo yanafaa kutafuta leseni na sheria za kudhibitisha ni watu wa umri gani wanapaswa kuangalia filamu fulani kutoka kwa bodi hiyo.

“Magari ya umma sio vituo vya sinema na hivyo wamiliki wa magari hayo wanapaswa kufuata sheria. Pili, filamu zote zitakazoonyeshwa zinafaa kuwa zile ambazo kila mtu hata watoto wanaweza kuzitazama. Pia, zinafaa kuendana na tamaduni, heshima na maadili yetu,”Dkt Mutua aliongeza.

Bodi hii iliwaomba wananchi kupiga ripoti kwa pale ambapo gari ambayo wanasafiria inaonyesha filamu chafu.

Pia, walitoa nambari ya dharura kwa umma ambayo watatumia kutuma ujumbe wa SMS au katika mtandao wa WhatsApp; nambari ya usajili wa gari, chama chake cha ushirika (Sacco), barabara inayotumiwa na ikiwezekana, video fupi ikionyesha filamu hiyo.

Aonya madereva

Dkt Mutua alionya madereva wanaoendesha magari ya shule dhidi ya kusikiliza stesheni za redio ambazo zinapeperusha vipindi vya watu wazima.

Aliwaomba wazazi na walimu kuunga mkono juhudi za bodi hii za kuhakikisha watoto wanalindwa kutokana na filamu ambazo zinaweza kuharibu maadili yao.

“Baadhi ya vituo vinapeperusha vipindi vya watu wazima na si vizuri watoto kusikiliza. Nambari ya dharura ni +254 748184499,” aliongeza.

Hata hivyo, aliwapongeza madereva na makondakta ambao wanafuata sheria na kuhakikisha kuwa abiria wanahudumiwa kwa heshima na wanasafiri vizuri na kusema kuwa watatuzwa.

“Tutasaidiana na wananchi  kuhakikisha kuwa wametuzwa vizuri  na pia tutawachagua wawe  mabalozi wa kuonyesha kuwa ni vizuri watu kutazama filamu safi. Maelezo ya jinsi watatuzwa yatatolewa,” Dkt Mutua alisema.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi viongozi na watumiaji mitandao ya kijamii wamepokea...

NGILA: Kenya ifuate mfano wa Israeli kuleta maendeleo

adminleo